Yanga wa Kimataifa Wafanya Kweli na Kuiondoa Simba Kileleni


Yanga wa Kimataifa Wafanya Kweli na Kuiondoa Simba Kileleni

YANGA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sifa nyingi kwa mfungaji wa bao hilo, Mzambia Obrey Chirwa dakika ya 70 baada ya kumtoka beki wa Azam FC, Mghana Yakubu Mohamed kufuatia pasi ndefu ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa kike mwenye beji ya FIFA, Deonesya Rukyaa wa Kagera, Yanga ilipata pigo dakika ya 30 baada ya kiungo wake Mzambia, Justin Zulu kuumia mguu wa kushoto na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake kuchukuliwa na winga, Emmanuel Martin.

Zulu aliwekewa mguu na kiungo wa Azam FC, Himid Mao wakati anapiga shuti kuunga mpira uliorudi baada ya kuokolewa kufuatia krosi ya kiungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda.
Martin alikwenda kucheza wingi ya kulia na Niyonzima akahamia katikati kuchukua nafasi ya Zulu aliyekuwa akicheza kama kiungo mchezeshaji.

Mabadiliko hayo ambayo hayakuwa mipango ya mwalimu, yaligeuka msaada mkubwa kwa timu hiyo, kwani Niyozima alikwenda kucheza vizuri sehemu ya katikati ya Uwanja na Yanga ikaanza kushambulia.

Azam nao wakapata pigo dakika ya 43 baada ya mshambuliaji wake, Yahya Mohammed kuumia msuli baada ya kupiga shuti na kushindwa kuendelea nafasi yake ikichukuliwa na Mghana mwenzake, Samuel Afful.

Kipindi cha pili, timu zote zilirudi vizuri na zikaendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa baada ya Yanga kupata bao dakika ya 70, wakaanza kucheza kwa kupoteza muda.

Ushindi huo unaifanya Yanga sasa ifikishe pointi 56 baada ya kucheza mechi 25 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ikiwaangushia nafasi ya pili mahasimu wao, Simba SC ambao kesho watacheza mechi ya 25 pia dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi 'Dida', Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Vincent Bossou, Nadir Haroub 'Cannavaro', Said Juma 'Makapu', Simon Msuva/Juma Mahadhi dk90+2, Justin Zulu/Emmanuel Martin dk30, Obrey Chirwa, Deus Kaseke/Geoffrey Mwashiuya dk54 na Haruna Niyonzima.

Azam; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Daniel Amoah, Yakubu Mohammed, Himid Mao, Salum Abubakar 'Sure Boy', Frank Domayo, Yahya Mohmmed/Samuel Afful dk44, Shaaban Iddi/Bruce Kangwa dk75 na Ramadhani Singano 'Messi'/Joseph Mahundi dk69.


Comments