HISTORIA FUPI YA CHRISTIAN BELLA



HISTORIA FUPI YA CHRISTIAN BELLA

1555492_415319391934058_1699477778_n

NI kijana mtanashati, mwenye mbwembwe jukwaani na uwezo wa ajabu wa kuchezea sauti yake hata ikaleta raha ya kipekee kwa shabiki wa muziki anayemtazama na kusikiliza anachoimba.

Huyo si mwingine bali ni Christian Bella 'Obama', ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), anayejulikana pia kama 'Mfalme wa Masauti'.

Umaarufu wake umezidi kupanuka na kuongezeka siku hadi siku tangu alipoletwa nchini na mwanamuziki King Dodoo, kutokana na mashabiki kumkubali kwa kasi tungo zake moja baada ya nyingine.

Dodoo alianza 'kumtambua' Bella kwenye baadhi ya nyimbo zake na kukata shauri kumtafuta, ambako kwa mara ya kwanza alianza kuimsikiliza laivu kwenye nyimbo za albamu yao akiwa Nairobi, Kenya.

"Wakati huo tulitoa albamu nikiwa na bendi ya Chateau Du Soleil," anafahamisha Bella na kuongeza "Nilipojiunga na Akudo wimbo wangu wa kwanza ulikuwa ni 'Walimwengu si Binadamu'."

Lakini Bella alianza rasmi kujiingiza kwenye muziki tangu akiwa na umri wa miaka 15, ambapo alikuwa Kiongozi wa bendi hiyo ya Chateau, iliyokuwa inamilikiwa na swahiba wa mwanamuziki Papa Wemba, aliyemtaja kwa jina moja la Frank.

Hiyo ni baada ya kuanzia 'mchangani' kwa kujikusanyakusanya tu vijana mtaani na kuimba akiwamo Fally Ipupa aliyewaacha baadaye na kwenda kwa Koffi Olomide.

Akiwa na miaka 16, Bella naye alienda kutesti zali kwa Koffi na kukubaliwa, ambapo hata hivyo hakupewa nafasi ya kupanda jukwaani na kuishia kukaa benchi tu kwa kumuona hana uwezo.

"Hadi na jiungana Akudo, mawazo yangu yote yalikuwa ni kurudi kwa Koffi, ambako siku niliposikia bendi yake imesambaratika nikahisi sasa ndoto zangu zimetimia kwani nitapata nafasi kiulaini," anasema Bella.

Hata hivyo, kabla Bella hajafanya maamuzi ya kuondoka nchini kurudi kwa Koffi, alitokea rafiki yake akamshauri kuachia wimbo mwingine wa Kiswahili baada ya 'Walimwengu si Binadamu' ndipo aondoke.

Hicho ndio kilikuwa chanzo cha kibao 'YakoWapi Mapenzi' kilichokubalika kupita kiasi na kumfanya Bella abadilishe maamuzi yake ya kuondoka, ilikutazama mwelekeo wa soko la muziki hapa nchini.

Kwa upande mwingine hiyo ilitoa nafasi kwa ndugu yake, Zoe Bella kujiunga na bendi ya Koffi badala yake, naye kuamua kufuta kabisa mawazo ya kuondoka kwa kutoa wimbo watatu ambao ni 'Safari Sio Kifo'.

Hivi sasa Bella ni Kiongozi wa bendi ya Malaika Music ambayo maskani yake ni Mbagala Magenge Ishirini, jijini Dar es Salam na inayomilikiwa na Mkurugenzi Daniel Denga.

Malaika inayokusanya vichwa kama Adaya, Petit Mauzo, Pilu, Mico Bella, Chesco Vuvuzela, Yanick Soslo, Babu Bomba na Kadogoo Machine, ndiyo bendi inayofanya vizuri zaidi kwenye maonesho ya ukumbini hivi sasa.

Bila kuficha kitu, kufanya vizuri kwa Malaika kumetokana na 'ukali' wa Bella jukwaani, kwa sababu kazi nyingi zinazofanya vizuri ni zake na hata asipokuwapo pengo lake linaonekana.

Baadhi ya vibao vya Bella vinavyotamba kwa sasa ni kama vile; 'Nakuhitaji', 'Usilie', 'Msaliti', 'Hanitaki Tena' pamoja na 'Nani Kama Mama'.

Kufanya vizuri kwa kibao 'Nani Kama Mama', kumempa nyodo Bella ya kuandaa onesho maalum alilolipa jina la 'Usikuwa Mama', lililofanyika Agosti 29, ndani ya Mzalendo Pub, jijini Dar es Salaam na kufana vilivyo.

Mwenyewe anaweka wazi kuwa, aliamua kutunga wimbo 'Nani Kama Mama' baada ya kushuhudia hatua zote za mkewe kujifungua na kuthibitisha kuwa kweli mwanamke anatakiwa kuheshimika vilivyo tofauti na anavyochukuliwa.

Anasema, onesho la 'Usikuwa Mama' lilikuwa maalum kwa akina mama wote duniani, ambapo aliwaalika pia wakali kibao wanaotamba kwenye muziki wa Bongofleva akiwamo Ommy Dimpoz aliyeimba naye wimbo huo.

Mwaka 2012 Bella alienda nchini Sweden kwa mke wake ambaye alikuwa mbioni kujifungua hivyo alilazimika kubaki huko ili ashuhudie mtoto wake akizaliwa.

Akiwa huko ndipo alipotunga kibao 'Msaliti' ambacho alikituma Tanzania na kikafanya vizuri, aliporudi akawa mwanamuziki huru na kufanikiwa kualikwa kwenye maonesho yote ya Fiesta akiwa mwanamuziki pekee wa Dansi.



Comments

  1. Mimi binafsi ninamkubali Bella zaidi na zaidi na nimwanamuziki ambaye haishiwi mashahiri.

    ReplyDelete
  2. Vp Bella Ana uraia wa nchi mbili Tz na Congo?

    ReplyDelete
  3. Bella anafanya kazi nzuri Sana...Kenya tunamutambua sana

    ReplyDelete

Post a Comment