HISTORIA YA SINGLE MTAMBALIKE aka Richie Rich




HISTORIA YA SINGLE MTAMBALIKE aka Richie Rich

Richie-Single-mtambalike-cut-560
BILA shaka jina la msanii Single Mohammed Mtambalike 'Rich Richie' halina ugeni masikioni mwa wapenzi, mashabiki na wadau wa sanaa ya maigizo, tamthilia na filamu kwa ujumla. 

Hiyo inatokana na kuwa, Richie anayetaja siri ya mafanikio yake kuwa ni kuwa msikivu na kutojikweza kwa wengine, hususan mashabiki na wapenzi, ni kati ya wasanii waanzilishi wa michezo ya kuigiza ya kwenye luninga.

 Alianza kujipatia umaarufu mwaka 1997, alipokuwa akiigiza katika luninga ya ITV, akiwa na kundi lililokuwa likijulikana kama '4 For You', lililojumuisha wasanii wanne, wengine watatu wakiwa ni Bishanga, Aisha na Waridi. 

Katika mazungumzo aliyoyafanya na mwandishi wa habari hizi, Richie anabainisha kuwa, akiwa na '4 For You' katika ITV, aliweza kushiriki kucheza michezo mingi iliyogusa nafsi za mashabiki
na wapenzi mbalimbali.

 "Mwaka 1998, tuliamua kubadili jina la kundi letu na kuliita 'Nyota Ensemble', baada ya kuliona limekwisha kuwa kubwa, ambapo tulishawaongeza pia wasanii wengine kama JB, Monalisa na Natasha," anasema Richie.

 Richie anasema, mwaka 2000, Nyota Ensemble lilisambaratika, akaasisi kundi lingine lililotikisa vilivyo kwenye luninga ya CTN, lililojulikana kama 'Nyota Academia', akiwa na wasanii zaidi ya 30, ambao wote wametokea kuwa maarufu mno hivi sasa. 

Anawataja baadhi ya wasanii hao kuwa ni Vicent Kigosi 'Ray', marehemu George Tyson, Lomole Matovolwa 'Big', Abiola, Abdallah Kombora, Macklin Mdoe, Macha, Mjomba Fujo, Mobby Mpambala na Mack Legan Kipara wa Orijino Komedi.

 Richie anasema kuwa, mwaka 2002, alianzisha kundi la 'Kamanda Family' lililowaibua wasanii kama Issa Mussa 'Claude', Shija, John Lista, Haji Adam 'Baba Haji', Hashim Kambi, John Kallage, Ahmed Olotu 'Mzee Chilo' na Fatma Shimweta.

 "Ilipofika Juni, 2003, niliajiriwa na Kampuni ya kutengeneza majani ya chai, 'Chai Bora', hivyo nililiacha kundi la Kamanda mikononi mwa Baba
 Haji, nikaenda kuwajibika kama Meneja Masoko na Matangazo," anasema Richie.

Anasema kuwa, wakati huo alikuwa na Kampuni yake iitwayo 'Rich Richie Art Promotion' iliyokuwa na mkataba na Chai Bora tangu mwaka 2001, ambapo mwaka 2005, aliibadili jina Kampuni hiyo na kuiita 'Bulls Entertainment'.

 Richie anaeleza kuwa, Kampuni ya Rich Richie ilikuwa ikijihusisha na matangazo pekee, lakini alipobadili jina na kuiita 'Bulls' ikawa pia 
inajishughulisha na uandaaji filamu, kuuza na kukodisha wasanii na maonyesho.

Kadhalika, anasema kuwa, amekwishapata mafanikio mengi tangu ajitumbukize katika sanaa ya uigizaji. Kupitia kampuni yake ya Bulls ambapo,
amekuwa akipokea tenda kemkemu hizi na zile zinazomfanya awajibike kila uchao bila kupumzika.

"Miaka miwili hivi nyuma nilionekana kwenye filamu nne kabambe, ikiwamo moja ya kwangu mwenyewe, 'Skendo', inayotikisa sokoni hadi sasa, 
niliyowashirikisha Rose Ndauka 'Mamaa wa Bulls', marehemu Adam Kuambiana, Dk. Cheni, Mobby Mpambala, Faiza Ally na Barafu," anasema Richie. 

Anazitaja nyingine alizocheza akiwa ameshirikishwa kuwa ni 'Kimya',  'Perfect Man' pamoja na 'Zawadi ya Birth Day' inayoandaliwa na Kampuni ya Jerusalem Film Company, ambayo ameonyesha uwezo mkubwa akiwa amecheza kama 'Daniel'.

Mbali ya hizo, katika kipindi cha hivi karibuni, Richie ameshaonekana kwenye muvi nyingi ikiwamo 'Jesca', akiwa katika uhusika tofauti tofauti na kufanya vema zaidi.

Baadhi ya filamu nyingine alizowahi kucheza miaka ya nyuma zaidi ni 'Agano la Urithi', 'Kwa Heshima ya Penzi', 'Copy', 'Kindergarten' pamoja na zile nne za kwake mwenyewe ambazo ni 'Solemba', 'Swahiba', 'Mahabuba' na Stranger'.

Katika filamu nyingi anazoigiza, Richie huonekana akicheza kama kijana bitozi anayejisikia mno huku akijitahidi kuzipamba filamu hizo kwa mbwembwe na madoido haya na yale ya kibishoo, lakini mwenyewe anazungumziaje?

"Wengi ninapokutana nao huhisi kuwa, wamekutana na mtu anayejisikia kupita kiasi, hii inatokana na staili yangu ya uigizaji, lakini mimi
 si bitozi kabisa, si unaona hata hapa tulivyokutana na kadhalika hivi tunavyoongea?" ananiuliza akicheka Richie. 

Anasema, kuigiza kwake kama bitozi kunatokana na waongozaji wengi kupendelea kumvisha husika hiyo, ambako anadai ni kwa vile anavyomudu
 vilivyo kucheza nafasi hiyo ambayo wakati mwingine inamfanya jamii imuogope na kumtenga.

 Richie anayevutiwa zaidi na msanii wa Marekani, Denzel Washington anachukua fursa hii kuwaomba mashabiki pamoja na wapenzi wa filamu kuuchukulia uigizaji wake wa kisanii tu na si maisha halisi ya msanii husika.

 Huyo ndiye Single Mohammed Mtambalike 'Rich Richie', aliyezaliwa Oktoba 5, mwaka 1972, jijini Dar es Salaam na kubahatika kupata elimu ya msingi katika shule ya Mnazi Mmoja na ya Sekondari katika shule ya Al Hamain, zote jijini Dar es Salaam.

"Mimi naishi Mtaa Pangani Namba 21, nikiwa na familia yangu, ambayo ni mke wangu niliyedumu naye kwa zaidi ya miaka 14 sasa nikiwa nampenda
 mno, na watoto wawili; Prince(13) na Darien(7)," anasema Richie.




Comments