YANGA SC imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco jioni ya leo Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia.
Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inatolewa kwa mabao ya ugenini, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga wataumia zaidi kwa kutolewa na Zanaco, kwani bao la kusawazisha la Wazambia hao Dar es Salaam lililopatikana dakika ya 78 kupitia kwa mshambuliaji wake Mghana, Attram Kwame lilikuwa la kuotea.
Na pamoja na hayo, wachezaji wa Yanga walikuwa wamezubaa kusubiri wapinzani wao watoe nje mpira kiungwana (Fair Play) baada ya mchezaji mwenzao, Obrey Chirwa kuangushwa.
Siku hiyo, Yanbga ilitangulia kwa bao la winga Simon Happygod Msuva dakika ya 39 baada ya kuwachambua mabeki wa Zanaco kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mzambia, Justin Zulu.
Na ushindi huu unaifanya Zanaco iendeleze rekodi ya kuitupa nje Yanga kwenye michuano ya Afrika, baada ya mwaka 2006 pia kuwatoa katika hatua kama hii ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 3-2, wakishinda 2-0 Lusaka baada ya kufungwa 2-1 Dar es Salaam.
Yanga sasa itamenyana na timu iliyofuzu hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho kuwania tikeit ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, wakati Zanaci inakwenda moja kwa moja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Comments
Post a Comment