Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Botswana Peter Butler amekiri kuwa, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anaekipiga kwenye klabu ya KRC Genk Mbwana Samatta alikuwa mwiba kwenye safu yao ya ulinzi na kusababisha matatizo makubwa.
"Alisababisha matatizo mengi kwenye safu yetu ya ulinzi, amefunga magoli mawili na alionesha kiwango kikubwa kiasi cha kusababisha mabeki wetu kumfanyia faulo nyingi baada ya kupata wakati mgumu wa kumdhibiti," anasema kocha wa Botswana baada ya kuulizwa ni mchezaji gani wa kitanzania ambaye alikuwa hatari kwenye timu yao.
Samatta alifunga magoli yote yaliyoipa Stars ushindi wa magoli 2-0 nyumbani dhidi ya Botswana kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa kwenye uwanja wa taifa.
Mbali na kufunga magoli mawili, nahodha huyo wa Stars alitengeneza nafasi nyingi za kufunga ambazo zingezaa magoli kama wachezaji wenzake wangekuwa makini zaidi kwenye eneo la hatari. Samatta pia alipiga ,mashuti kadhaa yaliyolenga goli lakini yaliokolewa na golikipa wa Botswana Kabelo Dambe.
Comments
Post a Comment