Sababu 3 za kiufundi zilizofanya Mayanga ampange Nyoni kwenye kikosi cha kwanza vs Botswana



Sababu 3 za kiufundi zilizofanya Mayanga ampange Nyoni kwenye kikosi cha kwanza vs Botswana

Kocha mkuu kwa sasa wa Taifa Stars Salum Mayanga ametoa ufafanuzi wa kiufundi kwa nini amemjumuisha Erasto Nyoni kwenye kikosi cha taifa baada ya watu kuhoji kwa nini aitwe wakati hajapata nafasi ya kucheza kwa muda kwenye kikosi cha Azam FC.

Mayanga ametoa sababu tatu (3) za kiufundi zilizomfanya akamteua Nyoni kujumuika kwenye timu ya taifa ikiwa ni pamoja na kumuanzisha kwenye kikosi cha kwanza cha Stars kilichocheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Botswana na kushinda 2-0.

"Sabu ya kwanza ya kumuita Erasto Nyoni ni kwa sababu namuamini kiufundi ndio maana nimemuita, sababu ya pili ya msingi nina idadi kubwa ya vijana kwenye eneo la nyuma kwa hiyo nilihitaji kuwa na mtu mzoefu,  sababu ya tatu, Erasto anaweza kucheza zaidi ya nafasi moja kwenye timu. Hivyo ndivyo vitu vilivyo sababisha   nimwite Erasto Nyoni."

"Tunapoita vijana naomba tuwape moyo tusiwakatishe tama kwa sababu hii ni timu ya wachezaji wote wa Tanzania, mwalimu anaagalia anaweza akamwita nani akasaidia nchi. Kwa hiyo naomba tuungane wote katika hilo."

"Hata tusinge shinda au tungefungwa kabisa, wachezaji bado walicheza vizuri kwa kujituma. Naomba watu watuachie vitu vya kiufundi lakini pale tutakapohitaji maoni kutoka wapenzi, vyombo vya habari, viongozi na wengine tutatoa nafasi hiyo."

Erasto Nyoni alicheza sambamba na Abdi Banda kwa dakika 90 katika nafasi ya beki ya kati kwenye mechi dhidi ya Botswana na kufanikiwa kumaliza mchezo huo bila kuruhusu goli.



Comments