GWIJI la upulizaji Saxaphone, Rashid Pembe limefichua kuwa "Mondinde" ndio albamu pekee ya Vijana Jazz ya enzi zake ambayo ilikosa msisimko kwa mashabiki kiasi cha kuwafanya wakimbiwe na kukebehiwa, licha ya kukusanya vibao ambavyo binafsi waliamini vingetingisha.
Albamu hiyo iliyotoka mwishoni mwa miaka ya 80, inabeba vibao sita vikiwemo vile maarufu vya "Masaki", "Na Nani" na chenyewe, "Mondinde".
"Nakumbuka wakati wa albamu ile ndio ndio muda huohuo tulikuwa tumepata vyombo vipya ikiwa ni pamoja na Drums za umeme, lakini hata zilipopigwa na kulia kwa mbwembwe, bado mashabiki walitucheka na kutuona washamba," amesema Pembe.
Amesema kuwa, walikuwa wakipiga na kuambulia watu wachache tu ambapo wengine wote walikuwa wakiwapita na kwenda kwenye bendi nyingine ikiwemo Maquis, tena huku wakiwacheka na kuuita ukumbi wao wa Vijana kuwa ni "banda la watoto".
Amesema kuwa kilichokuja kuwaokoa ni pale walipopata akili ya haraka ya kufyatua albamu nyingine ili kuepuka kuporomoka zaidi, ambapo kweli mashabiki waliwaitika upya mara tu walipoanza kuzisikia nyimbo kwenye kipindi cha "Misakato" cha RTD wakati huo.
Comments
Post a Comment