Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika timu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta jana ameing'arisha Taifa Stars kwa kuifungia mabao mawili na kuipa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana.
Mchezo huo wa kirafiki wa Kimataifa ulio katika kalenda ya FIFA, umepigwa katika dimba la Taifa Dar es Salaam na kushuhudiwa na maelfu ya watanzania wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe alikuwa mgeni rasmi, akiambatana na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye.
Katika mchezo wa leo ambao umejumuisha kikosi kipya kabisa cha Taifa Stars, chini ya kocha mpya Salum Mayanga, kimeanza kwa kasi ya aina yake na kufanikiwa kupata bao la mapema kabisa kunako dakika ya 2 mchezo kupitia kwa nahodha Mbwana Samatta aliyeitendea haki pasi ya Mohamed Hussein.
Taifa Stars iliendelea kuonesha kandanda safi, licha ya ubora na uimara wa Botswana, lakini ikashindwa kutumia nafasi kadhaa ilizopata kupitia kwa Samatta, Ajibu na Msuva.
Kipindi cha pili kilianza kwa Botswana kuongea nguvu na kufanya mashambulizi mengi ambayo hata hivyo ukuta wa Taifa Stars uliokuwa ukiongozwa na Abdi Banda, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein na Shomary Kapombe uliweza kutulia na kuhimili.
Mabadiliko ya kuwatoa Shiza Kichuya, Frank Domayo, Ibrahim Ajibu na Himid Mao na nafasi zao kuchukuliwa na Farid Musa, Mzamiru Yasin, Salum Aboubakary na Jonas Mkude, yaliweza kuzaa matunda ambapo katika dakika ya 77 Mwana Samatta akaifungia Taifa Stars bao la pili kwa mpira wa adhabu alioupiga baada ya kuangushwa nje kidogo ya eneo la 18.
Hadi mwisho wa mchezo, Tanzania inaondoka na ushindi wa mabao 2-0, ushindi ambao una faida katika viwango wa vya ubora ambavyo hutolewa naFIFA kila mwezi.
Comments
Post a Comment