KAMA ULIKUWA HUJUI... KIBAO "SIWALAUMU WAKWE" CHA MLIMANI PARK SIKINDE NI "DONGO" KWA REHEMA TAJIRI NA BABA YAKE MZEE JANJA



KAMA ULIKUWA HUJUI... KIBAO "SIWALAUMU WAKWE" CHA MLIMANI PARK SIKINDE NI "DONGO" KWA REHEMA TAJIRI NA BABA YAKE MZEE JANJA
SIRI ya kuwa kibao "Siwalaumu Wakwe" cha Mlimani Park Sikinde ni tukio la kweli, imefichuka hivi karibuni baada ya mwimbaji mahiri Rehema Tajiri kuhojiwa na mtangazaji Rajab Zomboko wa kipindi cha Afro Tz na kuweka bayana kila kitu.

Kwenye moja ya mfululizo wa kipindi hicho kinachorushwa na Radio One, Rehema alisema hivi karibuni kuwa kibao hicho kilitungwa na Max Bushoke aliyekuwa mpenzi wake kwa wakati huo, baada ya kukataliwa barua ya posa na baba mkwe wake, marehemu Hamis Tajiri.

Rehema alisema kuwa, mzee Tajiri alikataa Bushoke asimuoe kwasababu ya tofauti ya dini zao, sifa mbaya ya kabila la Max la Kihaya kwa wakati ule, ukorofi pamoja na ulevi wa kupindukia aliokuwa nao.

"Nakumbuka Max alikitunga kibao hicho kule kwenye jumba lao la DDC ya Mlimani tukiwa tumekaa na nikiwa sina hili wala lile, tena huku akiniambia kuwa anaamua kumweleza ukweli baba yangu," alisema rehema.

Alisema kuwa, awali alifikiri Max anatania lakini alikuja kubaini kwamba alikuwa ameamua baada ya siku nyingine baadae kuingia kwenye dansi la Sikinde DDC Kariakoo na kusikia kibao hicho kikitambulishwa kwa mashabiki.


Rehema alisema kuwa, baada ya kibao hicho kurekodiwa na kuanza kusikika radioni, mzee Tajiri aligundua kwamba amepigwa "dongo" na Max lakini aliishia kumwambia bintie tu kuwa anaelewa kila kitu kuhusu wimbo huo. 


Comments