Simba waomboleza kifo cha shabiki aliyefariki kwa goli la Kichuya



Simba waomboleza kifo cha shabiki aliyefariki kwa goli la Kichuya

UONGOZI wa klabu ya Simba umesikitishwa na kifo cha shabiki wa timu hiyo Elius Mweta aliyefariki dunia kwa mshituko baada ya winga Shiza Kichuya kufunga bao la ushindi kwenye mchezo wa watani wa jadi uliopigwa juzi katika uwanja wa Taifa.

Mweta alifariki dunia baada ya kushangilia kwa nguvu hali iliyomfanya kupata mshituko wa moyo na kuanguka chini kabla ya kupoteza maisha muda mfupi baadae.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Hajji Manara alisema uongozi umesikitishwa na msiba wa shabiki huyo na wanaungana na familia ndugu jamaa na marafiki katika kumuombea marehemu kwakuwa kila mmoja atapita katika njia hiyo.

"Tumesikitishwa sana na msiba wa shabiki wetu tunaungana na ndugu jamaa na familia katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo tukimuombea ndugu yetu apumzike kwa amani na uongozi wa Simba tunaangalia jinsi ya kupeleka rambirambi zetu," alisema Manara.

Marehemu Mweta atazikwa kesho saa 10 alasiri kwenye makaburi ya Kawe huku uongozi ukiyataka matawi yote ya klabu hiyo kwa jiji la Dar es Salaam kuperusha bendera nusu mlingoti siku ya kesho kumpa heshima shabiki huyo.

Wakati huo huo Manara alisema kikosi cha Simba kimeingia kambini hii leo tayari kuivutia kasi timu ya Mbeya City kwenye mchezo wa ligi ya Vodacom utakaofanyika kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam Jumamosi ijayo.

Simba wanaingia kwenye maandalizi ya mchezo huo wakiwa na morali ya hali ya juu kutokana na ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya wapinzani wao wa jadi Yanga juzi na kuwazidi pointi tano kwenye msimamo wa ligi.

Chanzo: Boiplus Media



Comments