Mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza ndiye aliyepewa jukumu la kuamua mchezo wa Simba na Yanga siku ya Jumamosi February 25, 2017 akisaidiwa na line one Mohamed Mkono (Tanga) na line two Hassan Zani (Arusha).
Akrama aliwahi kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa ligi kuu baada ya kuvurunda kwenye mchezo namba 80 wa Yanga vs Simba uliochezwa October 3, 2012.
Mechi hiyo ya mwaka 2012, Simba na Yanga zilitoka sare kwa kufungana goli 1-1 ilishuhudiwa Akrama akimtoa nje kwa kadi nyekundu Simon Msuva kwa kumchezea vibaya beki wa Simba wakati huo Juma Nyoso.
Siku tatu baadae (October 6, 2012) kamati ya ligi wakati (huo) ikatangaza kuondoa Akrama kwenye orodha ya waamuzi wa ligi kuu kwa kushindwa kumudu mchezo aliopangiwa.
Kuelekea mechi ya Jumamosi ijayo, TFF ilificha jina la mwamuzi atakaechezesha mchezo huo kwa sababu mbalimbali hali iliyopelekea kuibua tafsiri tofauti miongoni mwa wadau wa soka nchini.
Ikumbukwe, mchezo uliopita wa Yanga vs Simba (October 1, 2016) ulimalizika kwa vilabu hivyo kutoshana nguvu kwa kufungana goli 1-1 na kushuhudia mwamuzi Martin Saanya amkimtoa kwa kadi nyekundu nahodha wa Simba Jonas Mkude ambayo baadae ilifutwa.
Saanya aliishia kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa VPL msimu huu akidaiwa kushindwa kuumudu mchezo huo.
Comments
Post a Comment