KICHUYA AIING’ARISHA SIMBA PUNGUFU, YANGA ZEMBE YAPIGWA 2-1



KICHUYA AIING'ARISHA SIMBA PUNGUFU, YANGA ZEMBE YAPIGWA 2-1
WINGA Shiza Ramadhani Kichuya, kwa mara nyingine leo ameibuka shujaa wa Wekundu wa Msimbazi baada ya kutokea benchi na kuisaidia Simba kushinda 2-1 dhidi ya mahasimu, Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kichuya aliyempokea beki Novatus Lufunga dakika ya 55, kwanza alimsetia mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo kuifungia bao la kusawazisha Simba dakika ya 66 kabla ya yeye mwenyewe kufunga la ushindi dakika ya 81.
Ikumbukwe Kichuya ndiye aliyeifungia Simba bao la kusawazisha dakika ya 86 Oktoba 1, mwaka jana timu hizo zikitoka sare ya 1-1 baada ya Amissi Tambwe kutangulia kuifungia Yanga dakika ya 26 kwa makosa ya Lufunga tena.
Na leo Yanga SC walitangulia kwa bao la mapema tu dakika ya tano la Simon Msuva kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo Mzambia, Obrey Chirwa kuangushwa kwenye boksi na Lufunga.

Shiza Kichuya akiwa amebebwa juu baada ya kuifungi Simba bao la ushindi

Obrey Chirwa akimtoka beki Novaty Lufunga leo kabla ya kuangushwa na kusababisha penalti

Laudit Mavugo akimiliki mpira mbele ya beki wa Yanga, Kevin Yondan

Haruna Niyonzima akigombea mpira na Janvier Bokungu

Amissi Tambwe akiwa chini baada ya kugongana na Lufunga

Refa asiyejiuliza mara mbili katika maamuzi yake, Methew Akrama wa Mwanza alimtoa nje kwa kadi nyekundu beki Mkongo wa Simba, Janvier Besala Bokungu dakika ya 55 baada ya kumuonyesha kadi ya pili ya njano kufuatia kumchezea rafu Chirwa.
Akrama alikuwa mwiba kwa timu zote mbili leo kutokana na maamuzi yake ya kufuata sheria 17 za soka bila kusita pale tu linapotokea kosa, hali ambayo ilisababisha wachezaji wenyewe waamue kuwa na nidhamu uwanjani.
Yanga ndiyo waliuanza vizuri mchezo huo wakitawala sehemu ya kiungo, iliyokuwa ikiundwa na wageni watupu, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na Mzambia Justin Zulu.
Na Simba iliyonza na washambuliaji watatu, Mavugo, Juma Luizio na Ibrahim Hajib ikajikuta imeelemewa mno katika dakika 30 za mwanzo za mchezo.
Yanga watajilaumu wenyewe kwa kucheza mchezo wa 'kibishoo' zaidi, wakigongeana pasi zisizo na tija badala ya kusaka mabao moja kwa moja.
Kibao kilianza kuigeukia Yanga baada ya kocha Joseph Omog kumpunguza mshambuliaji mmoja, Luizio na kumuingiza kiungo Said Hamisi Ndemla dakika ya 27 aliyekwenda kuipa uhai timu yake.
Na Yanga ikapata pigo baada ya kiungo wake tegemeo, Kamusoko kuumia na kumpisha Said Juma 'Makapu'.
Kipindi cha pili, Simba SC ilirudi na maarifa mapya na pamoja na mabadiliko mengine yaliyofanywa na Omog, akiwatoa Lufunga na Mohammed Ibrahim na kuwaingiza Mkude na Kichuya mambo yakawa mazuri upande wao.
Pamoja na kumpoteza Bokungu aliyetolewa kwa kadi nyekundu, lakini Simba wakatoka nyuma na kushinda 2-1.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munishi 'Dida', Juma Abdul, Mwinyi Haji, Andrew Vincent, Kevin Yondan, Justine Zulu/Juma Mahadhi dk78, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko/Said Juma 'Makapu' dk45, Amisi Tambwe/Deus Kaseke dk70, Obrey Chirwa na Haruna Niyonzima.
Simba SC; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Novaty Lufunga/Shiza Kichuya dk51, Abdi Banda, James Kotei, Ibrahim Hajib, Muzamil Yassin, Juma Luizio/Said Ndemla dk27, Laudit Mavugo na Mohammed 'Mo' Ibrahim/Jonas Mkude dk57.


Comments