AWALI zilikuwa ni kelele za mashabiki wa Liverpool tu kwamba kikosi chao ni bora lakini kina makipa wa "kawaida" sana.
Kocha Jurgen Klopp hakufanya uamuzi wowote wa kusajili kipa wa kutisha katika Ligi Kuu inayoendelea nchini humo na sasa Liverpool imekuwa na makipa ambao wanaitwa "mashati" wakiwa golini.
Lakini juzi tu Klopp mwenyewe amekubaliana na madai ya mashabiki kwamba makipa wa timu hiyo ndio mchawi mkubwa wa matokeo mabovu.
Wiki iliyopita Liverpool ilipokea kipigo kutoka kwa Hull City na kudidimiza ndoto zao za ubingwa huku uwezekano wao wa kubaki kwenye nne bora nao ukiwa mdogo tofauti na mwanzo.
Klopp amewataja Simon Mignolet na Loris Karius magolikipa wa timu hiyo kwamba ndio chanzo cha matokeo yasiyoeleweka ndani ya Livelpool.
Mwanzoni Klopp alikuwa akimuaminia na kumtumia Mignolet lakini baadae kiwango chake kilionekana kushuka ghafla na kufungwa mabao ya kizembe.
Faulo iliyofungwa kwenye mechi dhidi ya Chelsea ilipunguza imani ya Klopp kwa Mignolet ambaye aliamua kumpa nafasi Karius lakini nae anaonekana kuwa mbovu.
Ikumbukwe mwaka jana Klopp aliingia katika majibizano na mchambuzi Garry Neville baada ya Neville kusema Klopp hana uchaguzi mzuri wa makipa.
Baada ya mechi ya Hull City aliulizwa kuhusu kipa wake na Klopp alisema: "Hilo ni tatizo letu kwa sasa na linatupa shida, sawa uwanjani hakuwa peke yake lakini unaweza kuona anavyokosa umakini, tuna tatizo golini kwetu."
Kocha huyo raia wa Ujerumani amesema kuwa anajua kwamba mashabiki wa Liverpool wanamwamini, lakini pia hawawezi kuendelea kuwa na imani nae kama timu inafungwa kizembe.
"Mimi ni kocha lazima kila mmoja anipende kwa kazi nzuri, watu wakisema wananipenda bado katika kazi mbaya itakuwa ni kituko. Lakini lazima niseme kwamba makipa wangu ni matatizo," amesema wazi kocha huyo.
Comments
Post a Comment