Maafande wa Tanzania Prisons wameetonesha kidonda cha 'mnyama' baada ya kumtandika bao 2-1 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Jumapili November 6, African Lyon walikata utepe wa vipigo kwa Simba baada ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mchezo ambao ulikuwa wa kwanza kwa Simba kupoteza tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
Simba ndio walikuwa wa kwanza kufunga bao dakika ya 44 likifungwa kwa kichwa na Jamal Mnyate aliyeunganisha krosi ya Shiza Ramadhani Kichuya.
Bao hilo liliipa Simba uongozi wa bao 1-0 hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili Tanzania Prisons walirejea vyema na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Victor Hangaya ikiwa ni dakika tatu tangu kuanza kwa kipindi cha pili. Hangaya aliunganisha pasi safi ya Kimenya ambaye ni beki wa kulia wa Tanzania Prisons.
Wakati Simba wakipambana kutafuta bao la pili, Prisons wakaongeza goli la pili na kuwa mbele kwa bao 2-1 dhidi ya Simba bao likifungwa dakika ya 63 na Victor Hangaya.
Dondoo
- Simba imepoteza mechi mbili mfululizo ndani ya siku nne na kuziachia pointi 6.
- Tanzania Prisons imeifunga Simba kwa mara ya pili mfululizo kwenye uwanja wa Sokoine. Msimu uliopita Prisons iliifunga Simba 1-0 (21/10/2015 Tanzania Prisons 1-0 Simba) kisha leo November 9 Prisons imeifunga Simba 2-1 kwenye uwanja huohuo mechi zote zikiwa ni za mzunguko wa kwanza.
- Angban ameruhusu magoli matatu kwenye mechi mbili mfululizo baada ya kucheza mechi sita bila wavu wake kuguswa.
- Tanzania Prisons wameshinda mechi yao ya kwanza baada ya kucheza mechi 4 bila kushinda. Mara ya mwisho Prisons walipata ushindi dhidi ya Stand United (19/10/2016 Tanzania Prisons 2-1 Stand United).
- Simba imepoteza mechi ya kwanza nje ya Dar, mechi ya kwanza Simba ilipoteza dhidi ya African Lyon, licha ya Simba kuwa mgeni kwenye mchezo huo bado walicheza jijini Dar kwasababu Lyon pia wanatumia uwanja wa Uhuru kama uwanja wao wa nyumbani.
- Simba imeendelea kusalia na pointi zake 35 kwenye ligi kuu Tanzania bara pointi tano mbele ya watani zao wa jadi Yanga, endapo Yanga itashinda mchezo wake wa kesho (Alhamisi November 10) itabakiza pointi mbili kuifikia Simba.
- Tanzania Prisons yenyewe imefikisha pointi 19 baada ya kufanikiwa kubakiza pointi tatu kwenye mchezo wao dhidi ya Simba.
- Simba iliifunga Mbeya City 2-0, Mbeya City ikaifunga Yanga 2-1, Yanga ikaifunga Tanzania Prisons 1-0 halafu Tanzania Prisons imeifunga Simba 2-1.
Comments
Post a Comment