Ball Boy anusurika kuchezea makofi kutoka kwa mchezaji wa Simba

img_4630

Kijana mmoja ambaye anaokota mipira (ball boy) kwenye uwanja wa Sokoine alinusurika kuchezea makofi kutoka kwa kiungo wa Simba Musa Ndusha baada ya dogo huyo kuchelewesha mipira kwa makusudi wakati Tanzania Prisons ikiongoza kwa magoli 2-1 dhidi ya Simba.

Mara kadhaa dogo huyo aliyekuwa nyuma ya goli la Tanzania Prisons alichelewa kurudisha uwanjani mipira ambayo ilikuwa imetoka nje ya uwanja hali iliyofanya golikipa wa Prisons kuchelewa kuanzisha mpira.

Ilibidi Ndusha aliyekuwa akifanya warm up nyuma ya goli la Prisons kwenda kumpa mpira golikipa wa Prisons wakati ball boy alikuwa na mpira miguuni lakini alikuwa akiuchezea tu kitu ambacho kinaashiria alifanya hivyo kwa makusudi na ilikuwa ni mpango maalum.

Tukio la ball boys kuchelewesha mipira lilijitokeza pia wakati wa mchezo wa Mbeya City dhidi ya Yanga Jumatano November 2, 2016 wakati Mbeya City wakiwa mbele kwa magoli 2-1.

Inaonekana ball boys wa viwanja vya mikoani wanapokea maelekezo kwamba, timu zao zinapokuwa zinaongoza wacheleweshe mipira.

Haruna Niyonzima pia aliwahi kumchimba mkwara kama si kutaka kumpiga ball boy wa uwanja wa Kambarage ambaye alikuwa akichelewesha mira wakati Stand ilipokuwa inaongoza kwa goli 1-0 dhidi ya Yanga September 25, 2016 kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Jumapili iliyopita November 6, kocha wa Stand United Athuman Bilal alilalamika kwenye vyombo vya habari kwamba, ball boys walikuwa wakichelewesha mipira kwa makusudi wakati timu yake ikiwa nyuma kwa magoli 2-1 dhidi ya Ndanda FC kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

"Hatukatai kufungwa lakini tufungwe huku tunacheza mpira, wakati mpira unaanza niliona mipira zaidi ya nane lakini tulipokuwa nyuma kwa magoli 2-1 mipira ikapungua nikanza kuona mipira miwili tu uwanjani," alilalamika Bilal huku timu yake ikiwa imelala kwa bao 2-1 dhidi ya Ndanda.

"Kipindi cha kwanza tulicheza vizuri lakini kipindi cha pili tulicheza kama dakika 15 tu kutokana na watoto kuchelewesha mipira kila ilipokuwa ikitoka nje ya uwanja."

TFF kupitia vyama vya soka vya mikoa inabidi kufanya uchunguzi wake na kuja na suluhisho ambalo litadhibiti vitendo kama hivi ambavyo siku moja huenda vikazua tafrani kati ya wachezaji na ball boys.



Comments