Na Baraka Mbolembole
AZAM FC imepoteza mchezo wa tatu kati ya minne ya mwisho katika ligi kuu Tanzania Bara msimu siku ya jana Jumatano.
Kipigo cha goli 1-0 kutoka kwa Stand United kimeiporomosha timu hiyo hadi katika nafasi ya nane ya msimamo wakiwa na alama 11 (pointi 9 nyuma ya vinara wa ligi Simba SC).
Mara ya mwisho timu hiyo kupata ushindi ilikuwa Septemba 10 baada ya kuifunga 2-1 Mbeya City FC katika uwanja wa Sokoine, Mbeya.
SAFU 'NYANYA' YA ULINZI
Si kawaida, katika misimu ya karibuni ambayo timu hiyo imefanikiwa kushinda ubingwa mara moja (2013/14) na kumaliza katika nafasi ya pili mara tatu (2012/13, 2014/15 na 2015/16) Azam ilikuwa na safu imara ya ulinzi.
Mlinzi huyo wa kati ameshindwa kuziba nyufa katika beki ya kati na kufanya makosa kadhaa ambayo yameigharimu timu yake. Aggrey alianza sambamba na Mwantika katika beki ya kati vs Stand na angalau timu ilicheza huku ikionekana kuwa na kiongozi katika beki.
Erasto ambaye ametoka katika majeraha alikuwa benchi na nafasi yake kuchukuliwa na kijana, Kangwa huku nafasi ya Kapombe katika beki mbili ikishikwa na Gambo.
Walinzi hao wa pembeni wameshindwa kupandisha mashambulizi kama ilivyokuwa ikifanywa na Erasto na Kapombe na jambo hilo limeipunguzia timu magoli.
Kuruhusu magoli 8 katika michezo 8 huenda isiwe tatizo, lakini kama timu haifungi magoli ya kutosha ni tatizo ambalo litaendelea kuwaangusha mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati.
BADO WANA SAFA
Katika kiungo, kocha Hernandez ameongeza sura mbili mpya, Thomas na Idd ambao wamekuwa wakipangwa sambamba na Bolou, Mugiraneza na Himid. Watano hao wamekuwa wakimchezesha mshambulizi pekee, nahodha, John Bocco.
Kuwapanga viungo watano bila kuwa na mpigaji wa pasi za mwisho ni jambo lingine ambalo limekuwa likiwagharimu Azam FC licha ya kwamba wamekuwa wakimiliki mchezo kwa wastani mzuri.
Salum Abubakary, Frank Domayo na Mudathir Yahya wameshindwa kupata nafasi mara kwa mara katika kikosi cha kwanza. Watatu hao ni wachezesha timu wazuri lakini inaonekana mbele ya kocha, Hernandez hawana nafasi. Wote walikuwa benchi vs Stand United sambamba na wing Ramadhani Singano.
Kiasi inashangaza sana kuona mwenendo huu wa Azam FC msimu hasa ukitazama aina ya wachezaji wao waliopo kikosini.
MASHAMBULIZI 'BUTU'
Azam FC imewapoteza, Kipre Tchetche, Allan Wanga, Didier Kavumbagu, Farid Musa na Ame Ally, lakini hawakufanya nyongeza ya usajili ya washambuliaji na badala yake wamebaki wakimtegemea zaidi nahodha, John Bocco pekee.
Hawakuwa makini hata kidogo katika usajili wao uliopita kwa maana unapowaacha washambuliaji watano kwa wakati mmoja na kushindwa kusajili walau wengine wawili ni tatizo.
Achana na mfumo wa uchezaji ambao umemfanya Bocco kucheza pekee, Azam ilipaswa kufanya usajili mpya wa washambuliaji ama kuwabakiza kikosini Kavumbagu au Ame ambaye wamempeleka kwa mkopo katika timu ya Simba.
Licha ya Bocco kufanikiwa kufunga magoli manne hadi sasa lakini idadi ya jumla ya magoli kumi ya kufunga katika game 8 ni ishara ya mambo kuanza kuwa magumu.
Walichapwa 1-0 na Simba, Septemba 17, wakapoteza 2-1 mbele ya Ndanda FC, Septemba 24, wakalazimishwa sare ya 2-2 na Ruvu Shooting, Oktoba 2, na sasa wamechapwa 1-0 na Stand. Mwishoni mwa wiki hii watacheza na mabingwa watetezi Yanga SC.
Hakika 'Wana Lamba-Lamba' wapo katika kipindi kigumu lakini ni lazima wakae chini na kujiuliza kuhusu mwenendo wao kama wanataka kurejea katika mstali na kushindania taji. Vipigo vitatu, mechi nne mfululizo pasipo ushindi, Azam FC inaelekea wapi?
Comments
Post a Comment