STRAIKA Robin Van              Persie amefunguka akisema kuwa angekuwa bado anakipiga              kwenye timu ya Manchester United endapo aliyekuwa kocha              wake, Alex Ferguson angekuwa bado anainoa klabu hiyo ya Old              Trafford.
        Jana staa huyo              raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 33, alikuwa akirejea              kwenye klabu yake ya zamani tangu alipoondoka Julai mwaka              jana na kwenda kujiunga na klabu ya Fenerbahce wakati timu              hizo zilipokuwa zikikutana kwenye mechi ya Ligi ya Europa.
        Katika kipindi              cha miaka mitatu aliyoichezea Man United, Van Persie aliweza              kuifungia mabao 58 na akafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu              England katika msimu wake wa kwanza ikiwa chini ya Ferguson.
        Baada ya hapo              straika huyo alicheza chini David Moyes na Luis van Gaal              kabla ya kuuzwa na anasema kuwa mambo yangekuwa tofauti kama              sio Ferguson angeondoka mwaka 2013.
        "Huwezi              kufahamu," staa huyo aliwaambia waandishi wa habari bada ya              kuhojiwa ni kitu gani kingetokea endapo Ferguson angekuwa              bado anaifundisha timu hiyo.
        "Ila ninachoweza              kusema pengine ningekuwa bado ni mchezaji wa Manchester              United. Wakati nasajiliwa sikuwa na mawazo kama Sir Alex              angebaki muda mfupi lakini kwenye soka kila kitu huwa              kinaweza kubadilika, huwezi kuweka mipango yako binafsi ama              kocha unayemtaka," aliongeza staa huyo.
        
Comments
Post a Comment