Nimeziwaza Yanga na Simba mara 10


Nimeziwaza Yanga na Simba mara 10

Yanga-makao makuu

1. Biashara ya soka inakua kila kukicha ndio maana hawa wawekezaji wamezitamani na sisi tumewapa kwa sababu tumechoshwa na wezi walikuwepo. Sio kwa sababu tumeridhika.

2. Tamaa ya mashabiki ni matokeo uwanjani, hili watalipata. Tamaa ya matajiri ni kutajirika zaidi, wamefanikiwa. Lakini kutakuwa na mstari katikati yao unaitwa klabu. Huu utaleta maswali siku za mbele juu ya nani auvuke kati ya hawa.

3. Kutokea namba mbili hapo ni kuwa, hakuna klabu inayomilikiwa na tajiri ambayo haijawahi kupitia misukosuko. Manji na Dewji walitakiwa walete mpango wa kuvifanya vilabu kuwa chapa inayoweza kujiendesha bila mifuko yao huku wakitajirika (thamani ya vilabu).

4. Kutokea namba tatu hapo, mifumo ya wote wawili imesimama katika biashara zao hawa wawili kuliko biashara za vilabu husika.

5. Natamani kutokea namba nne hapo watu tungetafakari maana ya neno nembo ya klabu kisha tujue namna gani inatakiwa kupewa thamani. Nembo sio ile pale kifuani, ile inawakilisha mashabiki milioni 3 na kuendelea wa kila klabu ambao ndio hasa hawa wawili wanawatafuta.

6. Sina tatizo na mfumo wowote kati yao. Biashara ni taaluma inayokua kila kukicha. Tatizo langu ni kuwa hatujathaminisha vilabu vyetu inavyotakiwa na wala hatujafahamu thamani yetu mashabiki.

7. Kutokea namba 7 ni kuwa, mashabiki hawajali thamani yao kwa sababu wameishi wengi ambao walinufaika na klabu kijanja na vilabu vimeishi muda mrefu bila mafanikio. Na hapa ndipo matajiri wataendelea kuwa sungura yaani wajanja.

8. Ieleweke tu kuwa kutokea namba 7 sina maana ujanja wao una athari hapana. Ni kuwa siku ambayo zitatokea Azam mbili nyingine Tanzania kama ilivyokuwa uwekezaji katika nchi nyingine, tutakuja kugundua kwanini Manji atakuwa tayari kupumzika na Mo atakuwa tayari kuuza timu huku kwenye akaunti zao kukiwa kumetuna huku kwingine kukisinyaa.

9. Kutokea namba nane ni kuwa, namaanisha mikataba yote imesukumwa na hisia za mashabiki na taratibu chanya kupuuzwa. Matajiri hawa wanavihitaji vilabu na vilabu vinawahitaji wao. Usawa ulitakiwa kuwepo.

10. Kutokea namba 9 ni kuwa usawa maana yake ni kuwa mahesabu sahihi ya ukodishaji na ununuzi yalitakiwa kufanyika. Hapa mashabiki tungekuwa tunacheka, matajiri wanacheka na klabu inacheka. Hii ndio mutual benefit. Nani kasema Manji atawekwa kwa miaka 10? Nani anajua kama ataiona Yanga kwa miaka 10? Ila Yanga itaishi milele na kuna watoto na wajukuu watahitaji kurithi Simba ambayo hisa zake ziliuzwa kiweledi na sio kwa hisia kurupushi.

Nicasius Nicholaus Agwanda (Coutinho Suso)

Soma Mwananchi kila Jumapili na jumatatu. Ukurasa unaitwa Gozi la ng'ombe.



Comments