Wataalamu wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), wanatarajiwa kutua nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kukagua Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Huu ni utaratibu wa CAF ambako baada ya muda hutembelea nchi wanachama kuangalia maendeleo ya miundombinu ya mpira wa miguu kabla ya kupandisha hadhi ya viwanja kwa ajili ya michuano ya kimataifa inayosimamiwa na kuendeshwa na CECAFA, CAF na FIFA.
Ukaguzi huo unafanyika wakati Tanzania inasubiri majibu ya Uwanja wa Sokoine wa Mbeya ambao ulikwiisha kukaguliwa na mapendekezo ya uboreshwaji kutolewa ili uweze kupandishwa hadhi ya matumizi ya kuchezwa mechi kubwa kama vile fainali za Kombe la Shirikisho, Ngao ya Hisani, michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mechi kubwa za kimataifa za kirafiki na mashindano ya CECAFA, CAF na FIFA.
Viwanja ambavyo CAF na FIFA inavitambua nchini Tanzania hadi sasa ni Amani wa Unguja, Zanzibar; Kaitaba wa Kagera, Azam Complex na Uwanja Mkuu wa Taifa vya Dar es Salaam.
Endapo CCM Kirumba utapitishwa, kutakuwa na nafasi ya kuruhusu kuchezwa mechi kubwa kama vile fainali za Kombe la Shirikisho, Ngao ya Hisani pamoja na mechi kubwa za kimataifa za kirafiki na mashindano ya CECAFA, CAF na FIFA.
Kirumba inaingia kwenye orodha ya viwanja vya Gombani ulioko Pemba; Sokoine wa Mbeya, Kaitaba wa Kagera ambavyo vilikwisha kukaguliwa na sasa vinasubiri kupitishwa ili kutumika kimataifa. Ujio wa viwanja hivyo, utapanua wigo wa Tanzania kuandaa michuano mikubwa katika ngazi ya timu za taifa kimataifa.
Imetolewa na TFF
Comments
Post a Comment