ZINEDINE ZIDANE AKUBALIKA REAL MADRID... mashabiki wapanga kumuaga kwa heshima atakapoondoka



ZINEDINE ZIDANE AKUBALIKA REAL MADRID... mashabiki wapanga kumuaga kwa heshima atakapoondoka
WAKATI kiungo fundi wa zamani, Zinedine Zidane raia wa Ufaransa akikabidhiwa mikoba ya ukocha wa mabingwa wa Ulaya, Real Madrid Januari mwaka huu, ni wadau wachache wa soka waliomkubali.

Wapo waliosema bora Madrid wangebaki na kocha wao Rafa Benitez kuliko kumpa Zidane kibarua hicho ambacho hana uzoefu nacho.

Kipigo cha mabao manne kwa bila kutoka kwa wapinzani wao wakuu, Barcelona kiliongeza joto kwa mashabiki lakini viongozi wa Madrid hawakutetereka, walimwamini Zidane na miezi mitano baadae akawapa ubingwa wa Ulaya kabla ya kuwaongezea taji la ubingwa wa Super League.

Hivi sasa mashabiki wa Real huaambii chochote kwa Zidane, wanaamini chini yake watarudisha enzi za mataji Santiago Bernabeu na wameshasema hata ikibidi kuondoka kwenye nafasi hiyo, watamuaga kwa heshima.

Zidane amefikia rekodi ya Pep Guardiola aliyeiongoza Barca kushinda mechi 16 mfululizo mechi za Ligi Kuu msimu wa mwaka 2010/11.

Real wanaongoza Ligi Kuu Hispania hadi sasa, walishinda mechi 12 mfululizo za mwishoni mwa msimu uliopita na msimu huu weshashinda mechi zote nne za kwanza.


Chini ya Zidane Madrid imecheza mechi 33, imepoteza mbili, imetoka sare tano na kushinda mechi 26 za michuano mbalimbali.


Comments