RANIERI AWASIHI MASHABIKI WA "THE FOX" KUMPOKEA KANTE KWA MIKONO MIWILI


RANIERI AWASIHI MASHABIKI WA "THE FOX" KUMPOKEA KANTE KWA MIKONO MIWILI
KABLA ya Leicester City kucheza na Chelsea, meneja wa klabu hiyo, Claudio Ranieri aliwasihi mashabiki wa The Fox kumpokea kwa mikono miwili kiungo kutoka nchini Ufaransa, N'Golo Kante ambaye alirejea klabuni hapo akiwa na kikosi cha Chelsea.

Ranieri aliwasilisha ombi hilo kwa mashabiki kufuatia kikosi cha Chelsea kutarajia kucheza mchezo wa Kombe la Ligi (EFL) dhidi ya Leicester katika uwanja wa King Power.

Kante aliondoka klabuni hapo wakati wa usajili wa majira ya kiangazi na kujiunga na klabu ya Chelsea, jambo ambalo linachukuliwa na mashabiki kama aliisaliti Leicester ambapo bado ilikuwa inamwitaji katika kipindi hiki cha kutetea taji lao hilo.

"Ninafarijika kuona Kante anarejea tena hapa na nitampokea kwa furaha na bashasha kutokana na mahusiano yetu kuwa mazuri tangu nilipomsajili mwaka 2015 akitokea Caen."

"Ninataka kuona hata kwa mashabiki inakuwa hivyo kwa sababu Kante bado ni sehemu ya familia yetu, ambaye alionyesha kujituma na kupata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa Ligi msimu uliopita."

"Mashabiki wanapaswa kufahamu kwamba soka ni mchezo ambao una changamoto zake na wakati mwingine inakuwa ngumu kuamini kwamba mtu anaweza kukuacha katika kipindi unachomwitaji, lakini bado ninasisitiza Kante ni mwenzetu na tunapaswa kumuheshimu kwa kiasi kikubwa," alisema Ranieri.

Kante alikuwa mchezaji pekee aliyeamua kuondoka wakati wa majira ya kiangazi, huku wachezaji wenzake waliochangia mafanikio ya kutwaa ubingwa wa England msimu wa 2015/16, Jamie Vardy na Riyad Mahrez, wakikubali kusaini mikataba mipya.


Klabu ya Arsenal ilionyesha nia ya kutaka kuwasajili Jamie Vardy na Riyad Mahrez lakini bado msimamo wao ulidhihirisha mapenzi na Leicester City.


Comments