MAMBO hayaendi kama yalivyotarajiwa kwa Jose Mourinho ndani ya Manchester United.
Mshindi huyo wa mara mbili wa Champions League, alitarajiwa kuifanya United iwe tishio kama ilivyokuwa enzi za Sir Alex Ferguson aliyestaafu ukocha mwaka 2013.
Vipigo vya hivi karibuni kutoka kwa Manchester City, Feyenoord na Watford, vimefichua baadhi ya mapungufu yaliyokuwepo tangu enzi za Louis van Gaal aliyetimuliwa msimu uliopita.
Gazeti la The Sun la Uingereza linaandika mambo saba ambayo Jose Mourinho anaweza kuyafanya ili kuifanya United iwe tishio.
1. Kumpiga benchi Wayne Rooney
Gazeti hilo linasema licha ya historia kubwa aliyonayo nahodha Wayne Rooney kwa Manchester United, lakini uwezo mdogo anaouonyesha uwanjani hivi sasa, unaididimiza timu.
The Sun linaandika kuwa kumpiga benchi Rooney kutaleta uhai kwa Paul Pobga ambaye atakuwa na wasaa mzuri wa kucheza nyuma ya mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic.
2. Kumrejesha Bastian Schweinsteiger kwenye kikosi cha kwanza
Siku zote Mourinho amekuwa na tabia ya kuwatema baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa kwenye kila klabu mpya aliyokwenda ili kuonyesha kuwa yeye ndiye 'in charge'.
Ni mbinu nzuri na kumbukumbu zinaonyesha namna alivyokuwa akifanikiwa kupitia mbinu hiyo, lakini United inakosa kiongozi kwenye eneo la kati.
Mourinho anapaswa kumrejesha kwenye kikosi cha kwanza kiungo mkongwe Bastian Schweinsteiger ambaye uwezo wake si wa kubeza.
Si lazima aanze lakini anaweza kutokea benchi na kuisadia timu pale itakapokuwa kwenye wakati mgumu.
Pobga aling'arishwa na viungo wakongwe wa Juventus, kitu ambacho anaweza pia kufanyiwa na Schweinsteiger ndani ya Manchester United.
3. Kumuanzisha Marcus Rashford
Marcus Rashford ameonyesha uwezo wa hali ya juu ikiwa ni sambamba na kufunga magoli muhimu, amekuwa akibalisha kasi ya timu kila anapoingia na ni wazi kuwa anastahili kuanza katika kila mchezo hasa katika kipindi hiki ambacho Anthony Martial amekuwa kwenye kiwango duni.
4. Kumpiga benchi David De Gea katika EFL Cup
Hakuna ubishi kuwa David De Gea ni mmoja wa makipa bora duniani, lakini kitendo cha kuamini kuwa hagusiki na hana mpinzani Manchester United, kimekuwa kikimfanya abweteke na kuzalisha makosa kadhaa yasiyostahili.
Mourinho anastahili kumipiga benchi katika baadhi ya mechi (hususan mechi za EFL Cup) ili kumjengea changamoto ya ushindani, hatua itakayomfanya kipa huyo wa Hispania ajitume zaidi.
5. Kumchezesha Morgan Schneiderlin
Huyu ni mchezaji mwingine ambaye hakufurahia maisha Old Trafford chini ya Van Gaal – lakini ana vigezo vyote vya kuwa staa kwenye Premier League.
Wakati Mourinho anatwaa taji lake la mwisho akiwa na Chelsea, shujaa wake alikuwa ni kiungo mkabaji Nemanja Matic.
Schneiderlin aling'ara sana akiwa na Southampton na anaonekana ni mtu sahihi kwa aina ya soka la Mourinho.
Nidhamu yake ya mchezo, itamsadia sana kumpa uhuru Pogba ya kuzunguka uwanja mzima.
6. Kusaka beki mpya wa kulia
Antonio Valencia ameanza vema msimu na amekuwa akimudu nafasi ya beki wa kulia tangu enzi za Sir Alex Ferguson, lakini amekuwa na makosa kadhaa kwenye mchezo wake, hivyo Mourinho anahitaji beki shupavu atakayedhibiti mashambulizi yote yanayotokea kushoto.
7. Kutoyaanika makosa ya wachezaji
Mourinho amemshutumu vikali beki Luke Shaw kwa kudai alihusika na ujio wa baadhi ya magoli waliyofungwa na Watford.
Beki huyo wa kushoto amekuwa kwenye kiwango kizuri tangu arejee uwanjani msimu huu kufuatia kuvunjika vibaya mguu wake mwaka jana, hivyo anahitaji kuungwa mkono na kocha badala ya kushutumiwa.
Comments
Post a Comment