ZLATAN IBRAHIMOVIC ASEMA ANAVUTIWA KUCHEZA PAMOJA NA WAYNE ROONEY


ZLATAN IBRAHIMOVIC ASEMA ANAVUTIWA KUCHEZA PAMOJA NA WAYNE ROONEY
MSHAMBULIAJI wa klabu ya Manchester United, Zlatan Ibrahimovic amesema anavutiwa kucheza pamoja na nyota wa klabu hiyo, Wayne Rooney msimu ujao.

Staa huyo raia wa Sweden aliyenusa nyavu mara moja katika mchezo dhidi ya Galatasaray wakati Rooney akipachika mabao mawili katika ushindi mnono walioupata wa mabao 5-2 wiki iliyopita wakati wa mandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu nchini England.

Ibrahimovic alifanikiwa kucheza katika mchezo mahususi kwa heshima ya Rooney uliopigwa dhidi ya klabu yake ya zamani ya Everton usiku wa Jumatano kwa lengo la kusheherekea miaka 12 akiwa na mashetani hao.

"Nadhani kila mchezaji mkubwa anatamani kucheza na mchezaji mkubwa," aliongea Ibrahimovic katika mahojiano na MUTV.

"Hilo sio tatizo, tuko wachezaji 11 uwanjani sio wawili, lakini kocha ndio anajua nini cha kufanya. Lakini nikiwa na Rooney sioni tatizo lolote isipokuwa mafanikio tu."

"Nilizungumza haya miaka mingi iliyopita, mchezaji mzuri kwa straika mzuri ni Wayne Rooney. Anafanya jitihada nyingi si kwa faida yake binafsi bali hata kwa straika na timu nzima kwa ujumla. Hakika nina furaha sana kuwa ni miongoni mwa wachezaji wanaocheza pamoja."


United katika mchezo wao wa kwanza msimu ujao watakutana na klabu ya Bournemouth utakaopigwa Agosti 14.


Comments