HATA SIR FERGUSON ALITUMIA ‘MKWANJA MREFU,’ ACHA POGBA AVUNJE REKODI…


HATA SIR FERGUSON ALITUMIA 'MKWANJA MREFU,' ACHA POGBA AVUNJE REKODI…

Pogba-Man U-Juve

Na Baraka Mbolembole

MICHEZO 1500 ilitosha kwa Sir Alex Ferguson kutengeneza jina kubwa katika 'miongo' yake miwili na nusu pale Old Trafford. Wakati, Fergie alipoamu kustaafu ghafla mara baada ya kuipa taji la 13 na la 19 la kihistoria, United alikuwa na miaka 71.

Ilikuwa ni wakati mwafaka kwa yeye kustaafu lakini tangazo lake  lilikuwa ghafla mno Mei, 2013. Kama shabiki wa United kusema kweli sikupendezwa na uamuzi wake huo licha ya kuamini amewaacha 'wanafunzi wazuri' ambao wanaweza kuendeleza mafanikio ya klabu hiyo ya Old Trafford.

Wachezaji wa zamani kama Gary Neville, Phill Neville, Nicky Butt, Ryan Giggs, Rio Ferdinand na Paul Scholes  wote hawa nimepata kuwaona wakiitumikia United na nilikuwa na shahuku kubwa baada ya kuondoka kwa Ferguson kuona timu ikiangukia katika mikono yao.

Chaguo la David Moyes mwanzoni lilionekana si tatizo lakini miezi kumi baadae ilionekana kazi aliyopewa ilikuwa ni kubwa zaidi yake. Moyes alipokea kazi hiyo akitokea timu ya Everton ambayo alidumu nayo kwa miaka 11.

Alipotangazwa Moyes , Bodi ya klabu na Ferguson walisema kuwa walihitaji kuona Manchester United inakuwa chini ya mtu sahihi wa ufundi, zaidi walisema walihitaji 'mtu hasa wa United,' ndiyo maana wakamchagua, Moyes.

Ukweli, United walihitaji kocha Muingereza na Waingereza hawakutaka kuona timu hiyo ikiangukia kwa kocha wa kigeni. Makocha wengi wa Kiingereza walisema United itatetereka baada ya kuondoka kwa Ferguson lakini si Roy Keane, nahodha-kiongozi wa zamani wa timu hiyo ambaye hata Fergie mwenyewe amekuwa akimtaja sehemu ya mafanikio yake na klabu.

Keane angeweza kusema hadharani kuwa United haitatetereka licha ya Fergie kustaafu, japo ni kweli atakumbwa. Miaka mitatu akiwa nje ya benchi la ufundi la timu hiyo, Ferguson ni kama ameondoka na rekodi zake.

Miezi kumi ya Moyes ilikuwa ni migumu mno kwa mashabiki wa United kwa maana timu yao haikuwa na uwezo wa kushinda wiki nne mfululizo. Luis Van Gaal alikuwa ni kocha wa kigeni wa kwanza kuifundisha United mara baada ya kumalizika kwa fainali za kombe la dunia 2014 nchini Brazil.

Van Gaal ni chaguo ambalo  Waingereza wengi hawakulipenda. Achana na tabia yake ya kidikteta, Van Gaal alikuwa akikosolewa wazi hadi na wachezaji mastaa waliopita klabuni hapo. Stahili yake ya timu kupasiana sana na kutegemea mashambulizi ya kutokea katikati ya uwanja ilipigwa vita sana.

Ilifikia hatua ya Scholes kusema 'United inaboa.' Mholland huyu alipewa muda wa kutosha (misimu miwili) na mafanikio yake makubwa yanabaki kumaliza TOP 4 katika msimu wake wa kwanza ambao uliambatana na usajili wa rekodi England, 2014/15.

Kiungo-mshambulizi, Angel Di Maria alisajiliwa akitokea Real Madrid kwa ada ya pauni 60 milion. Pia, Van Gaal aliwasaini wachezaji kama Marcos Rojo, Dael Blind, Radamel Falcao na nyota hao wakamsaidia kuirudisha United katika ligi ya mabingwa Ulaya.

Msimu wa pili wa Van Gaal alifanikiwa kushinda taji la FA lakini alikuwa ni 'mshindwa' mwingine, huku yeye akikoselewa zaidi katika sera yake ya usajili. Van Gaal alitumia zaidi ya paun 225 milion katika sajili zake za wachezaji Old Trafford.

Wakati, Moyes alionekana kutoa-challenge katika kuwania mataji ya ndani akiwa na timu yenye bajeti ndogo-Everton, lakini kuwa kocha wa United hakukumfanya kusajili wachezaji wa gharama kubwa. Aliwasaini, Marouane Fellaini na Juan Mata pekee kwa ada ambayo hakuvuka paun 60 milion.

Kwa kuwa alijiunga na timu inayoongozwa na watu wa mpira na wenye mipango na uchumi mzuri, ilidhaniwa Moyes angepata mafanikio ndiyo maana alipewa kandarasi ndefu ya miaka sita.

Huwezi kusita kumpongeza kwa mipango yake mizuri kwa ligi ya England. Lakini katika michuano ya Ulaya hakuwa na mipango mizuri sana, ndiyo maana ameishia kushinda mara mbili tu taji hilo. Fergie alikuwa ni mtumiaji mzuri sana wa fedha, hakuna shaka kuwa alikuwa na vikosi imara muda wote, lakini mara nyingi alifanya usajili wa fedha nyingi na kuwalipa mishahara mikubwb wachezaji wake.

Keane, Dwight Yorke, Jaap Stam, Ruud Van Nistelrooy, Rio, Juan Sebastian Veron, Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney, Michael Carrick, Owen Hargreaves, Luis Nani, Dimitar Berbatov, Antonio Valencia, Criss Smalling, Phill Jones, Wilfred Zaha, David De Gea, na wengine hivyo hata Van Gaal alikuwa sahihi katika matumizi japo ni kweli alitumia kiasi kikubwa mno ndani ya misimu yake miwili.

Matumizi makubwa ya pesa za usajili bado yanaendelea Manchester United na ikiwa dili la Paul Pogba litakamilika, kocha mpya Jose Mourinho atakuwa ameshatumia kiasi kisichopungua paundi 150 milion.

Ukichanga na zile alizotumia Moyes na Van Gaal, United itakuwa imetumia kiasi kikubwa mno cha pesa. Ndiyo maana baadhi ya wachambuzi wa kimataifa wamekuwa wakikosoa hata ada inayotarajiwa kutumia kumsaini Pogba (pauni 100 milion).

Usajili wa rekodi ya dunia unaweza kuisaidia sana United na mataji manne ya Serie A aliyoshinda Mfaransa huyo akiwa Juventus, kiwango na nafasi yake uwanjani na umri alionao ni wazi Pogba anakaribia thamani yake ya sasa. Acha tu, Mourinho atumie pesa kusaini wachezaji ambao anaona wataipasha tena Manchester United kwa maana hata Fergie alikuwa mnunuzi wa wachezaji wa gharama.

Jose awali alionekana si chaguo zuri (wakati Ferguson alipostaafu) lakini ni yeye sasa ambaye amebeba kila tumaini la shabiki wa United. Naamini, licha ya kwamba si mtu wa United, mbinu zake zitanaweza kuimarisha tena kiwango cha ushindani cha United. Hata Sir Ferguson alitumia 'mkwanja mrefu,' acha Pogba avunje rekodi…



Comments