BASTIAN SHWEINSTEIGER KUREJEA BAYERN MUNICH MSIMU HUU


BASTIAN SHWEINSTEIGER KUREJEA BAYERN MUNICH MSIMU HUU
NYOTA ambaye alisajiliwa kwa mbwembwe katika timu ya Manchester United lakini akawa hana nafasi kwa kocha Jose Mourinho, anatarajiwa kurejea katika klabu yake ya zamani.

Kiungo mzuri kabisa kwa kukaba na kusogeza mashambulizi, Bastian Schweinsteiger anatajwa kwamba anatarajiwa kujiunga na klabu yake ya zamani ya Bayern Munich msimu huu.

Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani alikuwa na wakati mbaya ndani ya Manchester United kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

Kibaya zaidi ni kwamba baada ya kocha mpya Jose Mourinho kuwasili katika kikosi hicho, amesema kwamba Mjerumani huyo ni miongoni mwa wachezaji ambao hawataki.

Kwa mujibu wa gazeti la michezo la Bild, ofisa mtendaji mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge amefungua milango kwa nyota huyo kurejea katika utamu wa Bavaria, mwaka mmoja tu baada ya nyota huyo mwenye miaka 32 kuungana na kocha wake wa zamani, Louis Van Gaal ndani ya Manchester.

"Yeye mwenyewe (Schweinsteiger), ameongea kuhusu maisha yake ya baadae ya kisoka na amedhani kwamba kurejea hapa ni wakati mwafaka," Rummenigge amekaririwa akisema.

Haifahamiki hata hivyo, Schweinsteiger ataweza kucheza wapi katika kikosi cha Bayern ambacho sasa kiko chini ya kocha mwenye mafanikio, Carlo Ancelotti.

Katika nafasi hiyo, tayari Bayern ina watu wa kazi kama Thiago, Javi Martinez, Xabi Alonso, Arturo Vidal na Renato Sanches wakati pia David Alaba na Philipp Lahm nao wanaweza kucheza kama viungo wa kiwango cha juu kabisa.

Lakini wakati Bayern wakiwa wanamsaka kwa udi na uvumba nyota wao uyo, gazeti la Manchester Evening limeandika kwamba klabu za AC Milan na Inter zote za Italia, zimetuma maombi ya kumsajili mchezaji huyo.

Schweinsteiger ameanza katika mechi 21 na mechi 10 kama mchezaji wa akiba katika msimu uliopita, ingawa kwa miezi minne amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya goti.

Chini ya uongozi wa Mourinho sasa Manchester United ni kama imeshafungua milango kwa klabu yoyote inayomtaka nyota huyo mkongwe

Comments