STAA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Thomas Muller ametoa onyo kali kwa wapinzani wao, Italia kuelekea mtanange utakaowakutanisha wababe hao wa dunia.
Ujerumani wataivaa Italia katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano ya Euro 2016, utakaopigwa kesho.
Nyota huyo anatoa mkwara huo huku akiwa hajapachika bao hata moja tangu kuanza kwa michuano hiyo inayoendelea nchini Ufaransa.
"Haijalishi nani anafunga, sijali kutofunga. Lakini nitachukua ubingwa," alisema Muller alipokuwa akihojiwa na mtandao wa Gazzetta dello Sport.
"Siwezi kuchanganyikiwa kwasababu sijapachika mabao. Nimekuwa nikifunga mara kwa mara."
Muller anaamini kuwa kikosi chake kiko sawa na amefurahi kukutana na Italia katika hatua hiyo ya mashindano.
Katika hatua nyingine, Muller amekiri kuwa mtanange huo utakuwa mgumu kwa timu zote, licha ya ukweli kwamba wamejipanga kuibuka na ushindi.
"Ndio, timu yoyote inaweza kupoteza mchezo. Watu wanasema kuwa Waitalia wanapenda kujiangusha na walalamikaji sana kwa waamuzi. Lakini nawapenda," aliongeza Muller.
Mshindi katika mchezo huo atakutana na aidha wenyeji Ufaransa au Iceland katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Comments
Post a Comment