THOMAS MULLER ASUSA KUPIGA PENATI



THOMAS MULLER ASUSA KUPIGA PENATI
STRAIKA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Thomas Muller ameweka wazi kwamba hataweza kupiga tena penati, baada ya majuzi kushindwa kuziona nyavu katika mechi ya robo fainali ya michuano ya fainali za mataifa ya Ulaya "Euro 2016" ambayo waliibuka na ushindi dhidi ya Italia.

Katika mchezo huo uliopigwa Jumapili usiku, mabingwa hao wa dunia walikuwa wakihitaji ushindi wa penati baada ya kwenda sare ya bao 1-1 na Italia katika muda wa dakika 120, lakini Muller ni mmoja kati ya nyota watatu wa Ujerumani waliokosa kuziona nyavu wakiwa yadi 12, baada ya shuti lake kuokolewa na mlinda mlango Gianluig Buffon.

Straika huyo mahiri vilevile aliwahi kuikosa penati wakati wa mechi ya Bayern Munich dhidi ya Atletico Madrid katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na sasa anaonekana kuamua kutopiga tena mipira hiyo.

"Sitapiga tena penati katika kipindi cha wiki mbili zijazo," Muller aliliambia jarida la Sport Bild.


"Nitajifunza mwenyewe kutafuta mbinu za kufunga penati na nitarejea nikiwa fiti katika kipindi vcha mwezi mmoja ama miwili," aliongeza.


Comments