STRAIKA Luis Suarez amesema kwamba ana uhakika staa mwenzake, kwenye kikosi cha Barcelona, Lionel Messi atarejea kukichezea kikosi cha Argentina siku zijazo.
Baada ya Jumapili kuambulia kipigo cha mabao 4-2 kwa mikwaju ya peneti Chile katika mechi ya fainali za Kombe la Copa America Centenario iliyopigwa kwenye uwanja wa Metlife, Messi ambaye alikosa penati alisema kuwa kazi ya kuichezea timu hiyo imemalizika.
Hii ni mara ya nne kwa nyota huyo mwenye miaka 29 kufungwa kwenye mashindano makubwa akiwa na timu hiyo na siku hiyo akashindwa kumaliza ukame wa miaka 23 wa nchi hiyo kushindwa kutwaa ubingwa.
Hata hivyo, Suarez ambaye anacheza na Messi katika timu ya Barcelona na msimu uliopita kuipa mataji mawili, anaamini kuwa staa huyo atabadili uamuzi.
"Ninavyomfahamu, leo alisema hivyo kutokana na majonzi na bila msaada," staa huyo wa timu ya taifa ya Uruguay alikiambia kituo cha radio Tenfield.
"Itakuwa ni aibu kwenye soka endapo atachukua uamuzi kama huo, lakini nina uhakika atabadili uamuzi," aliongeza straika huyo.
Alisema kwamba kipindi hicho kilikuwa ni kigumu kwa kila mtu na kila mmoja angeweza kutoa uamuzi na ukaheshimika.

Comments
Post a Comment