MARCOS ROJO AONJA JOTO YA MOURINHO... atemwa kikosini na kuambiwa "waweza kwenda kokote"





MARCOS ROJO AONJA JOTO YA MOURINHO... atemwa kikosini na kuambiwa "waweza kwenda kokote"
KILA kitu kina wema na ubaya wake, hata kwa upande wa binaadamu kuna atakayependwa na kuchukiwa.

Siku chache tu baada ya kukabidhiwa kibarua cha kuinoa Manchester United, kocha Jose Mourinho tayari ameonyesha kuwa ni mwiba mchungu kwa baadhi ya wachezaji aliowakuta ndani ya kikosi.

Beki Marcos Rojo ni kati ya wanandinga wanaoonja machungu ya kocha huyo raia wa Ureno, baada ya kutaarifiwa kuwa hayumo katika mpango wa kubaki katika viunga vya Old Trafford msimu ujao.

Kutokna na hilo, Mourinho amemfungulia mlango wa kutokea mwanandinga huyo raia wa Argentina.

Taarifa ya ndani ya klabu ya Manchester United inasema kuwa Rojo ameelezwa wazi aanze kusaka timu ya kukipiga msimu ujao na kwamba asikatae ofa za timu zinazomwitaji.

Tena katika mazingira ya kuhalalisha safari ya kuondoka, Mourinho ameweka bayana azma yake ya kukubali ofa ya klabu yoyote inayoanzia pauni mil 9.7 kwa ajili ya Rojo.

Lakini katika msemo wa "ukisema cha nini", tayari kuna taarifa za klabu mbalimbali kuhitaji huduma za mwandinga huyo kupitia usajili huu unaoendelea wa majira ya joto.

Taarifa za magazeti yaandikayo habari za michezo zimebainisha kuwa klabu za kutoka nchi za Hispania, Italia na China zimeonyesha nia ya dhati ya kupata saini ya Rojo katika kipindi hiki cha usajili.

Rojo alitua Old Trafford msimu uliopita huku akiwa anahitajika pia na timu kama Sporting Clube de Portugal, lakini aliamua kutua katika Ligi ya premier.


Tayari Mourinho ameshaanza usajili wa kuimarisha kikosi chake cha msimu ujao akiwa na mashetani wekundu wa jiji la Manchester kwa kumwita kikosini mlinzi wa Villarrel ya Hispania, Eric Bailly.


Comments