STAA Divock Origi amesema kuwa yupo kamili kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya kupigania namba kwenye kikosi cha Liverpool kinachonolewa na kocha Jurgen Klopp.
Nyota huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji na mshindani wake Cristian Benteke, wameshaungana na kikosi cha timu hiyo kilichowekwa kambini nchini Marekani kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao, baada ya kumaliza mapumziko waliyopewa baada ya kumaliza fainali za Euro 2016.
Katika kikosi hicho, Origin a Benteke wanajiandaa kukabiliana na mastraika Daniel Sturridge, Danny Ings na Roberto Firmino katika nafasi kwenye kikosi cha kwanza na huku wakitishiwa na mastaa wengine, Sadio Mane na Gerginio Wijnaldum.
Hata hivyo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 21, alisema jana kwamba yeye na wachezaji wenzake ni lazima wapambane ili kuhakikisha wanapata namba.
"Tupo kwenye klabu kubwa na hii ndio moja ya changamoto ya kuwa kwenye klabu kubwa. Na hii ndio huwa inakusukuma ili ufanye vizuri," alisema staa huyo kupitia tovuti ya klabu hiyo.
"Tunapaswa kusukumana na kusaidiana na kwa kufanya hivyo tunaweza kupata mafanikio," aliongeza nyota huyo.
Comments
Post a Comment