ANTONIO CONTE ADAI ALITENGWA ITALIA... asema hiyo ni siri nzito iliyoutesa moyo wake



ANTONIO CONTE ADAI ALITENGWA ITALIA... asema hiyo ni siri nzito iliyoutesa moyo wake
PUNDE tu baada ya kuaga michuano ya Euro 2016, kocha wa Italia, Antonio Conte amefichua siri nzito iliyomtesa moyoni mwake kuwa hakupewa sapoti ya kutosha katika kipindi cha miaka miwili aliyoifundishia timu hiyo.

Italia usiku wa kuamkia jana iliaga michuano hiyo hatua ya robo fainali kwa kulala kwa penati 6-5 mbele ya mabingwa wa dunia, Ujerumani.

Aliutumia mchezo huo kuaga rasmi kwa kuwa mkataba wake ulikuwa unamalizika baada ya kumalizika kwa michuano hiyo na juzi aliwaaga rasmi mashabiki na wachezaji wake, ikiwa ni mwanzo wa safari ya kujiunga na Chelsea.

Baada ya mchezo huo, Conte alisema alifanya kazi kivyakevyake hadi anaondoka kikosini hapo juzi bila ya kupata sapoti ya kutosha.

"Sikuona sapoti yoyote, vyombo vya habari ama mtu yoyote, yaani ilikuwa Conte dhidi ya jambo lolote," alisema na kuongeza:


"Siku zote nimekuwa nikipigania maslahi ya timu ya taifa na sio mimi binafsi. Kama nitakuwa mkweli, sikuwahi kuona sapoti niliyostahili kuipata."


Comments