WACHEZAJI 12 WENYE MAJINA MAKUBWA WALIOWAHI KUKOSA PENATI MUHIMU


WACHEZAJI 12 WENYE MAJINA MAKUBWA WALIOWAHI KUKOSA PENATI MUHIMU

penati

Naseem Kajuna

Inasemekana kwamba kupiga Penati ni moja ya vitu rahisi kwenye mpira ambacho mchezaji yeyote yule wa mchezo wa mpira wa miguu anapasa ajue.Mnamo dakika ya 54 ya mchezo wa jana kati ya Taifa Stars na timu ya Misri mchezaji  tegemezi wa Taifa Stars na klabu ya KRC Genk alikosa Penati ambayo ingeweza kuirudisha Stars kwenye mechi hiyo. Kitendo hiki kilinifanya niwaze kwanini mara nyingi wachezaji hukosa penati muhimu kwani Mbwana Samatta sie wa kwanza na wala hatokuwa wa mwisho kufanya hivi.

Hawa ni wachezaji  wengine 12 waliopata bahati mbaya ya kukosa penati muhimu.

SERGIO RAMOS

penati 1

Nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 kati ya Real Madrid na Bayern Munich ilishindwa kuzaa mshindi ndani ya dakika 90 na ata 30 za nyongeza na mechi hii ilienda hadi hatua ya matuta.Manuel Neur alifanya yake na akaweza kutoa penati mbili za Real Madrid zilizopigwa na Cristiano Ronaldo na Kaka.

Basi inaonekana Sergio Ramos alishindwa kuvumulia presha iliyoletwa na mashabiki wa Real Madrid siku hiyo ndani ya uwanja wa Santiago Bernabeu, maana alipaisha penati yake juu kabisa ya goli.Kitendo hichi kikamruhusu Bastian Shweinsteiger kupiga penati ya mwisho ya Bayern na kuiwezesha timu yake kufudhu kuingia fainali ya kombe hilo mwaka huo.

DAVID TREZEGUET

penati 2

Pale fainali ya kombe la Dunia inapoenda penati basi ni lazima angalau mchezaji mmoja atamani kuchimba shimo na kudumbukia mwishoni mwa mechi, lakini hakuna mtu alitegemea kama mwaka 2006 mchezaji huyu angekuwa David Trezeguet kutokana na Umahiri wake wa kumaliza aliouonesha kwa klabu zake mbalimbali na ata timu yake ya Taifa.

Waitaliano walishapata penati zao zote mbili walizopiga mpaka hapo ilipofika zamu ya Trezeguet kupiga mkwaju wake.Alipiga penati yake mwamba wa juu.kitendo hichi kiliigharimu Ufaransa kwani  Fabio Grosso alifanikiwa kufunga mkwaju wa mwisho wa Italia na kuwawezesha Waitaliano kushinda kombe la Dunia kwa mara ya tano katika historia yao.

JUAN ROMAN RIQUELME

penati 3

Riquelme ni moja ya namba 10 bora zaidi kuwahi kutokea kwenye mpira japo hakuweza kupata mafanikio ambayo kipaji chake kilistahili.Msimu wa 2005/2006 alisaidia timu yake ya Villareal kufika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya walipocheza dhidi ya Klabu ya Arsenal.Katika mechi ya pili ya mtanange huo huku Arsenal ikiwa inaongoza kwa goli moja Riquelme alipewa Penati ambayo ingeweza kupeleka mechi hiyo mda wa nyongeza

Mbele ya mashabiki wake Riquelme alitazama Penati yake iliopigwa Upande wa Kulia ya Goli ikitolewa na Kipa Mjerumani wa  Arsenal Jens Lehmann akiacha mashabiki wake wakisitika.

RAUL

penati 4

Nadhani ungewauliza mashabiki wa timu ya Hispania kuchagua mchezaji atakayepiga Penati ambayo ingeivusha timu ya Hispania hatua ya Robo fainali dhidi ya mabingwa wa Dunia wa wakati huo Ufaransa kwenye Michuano ya  Euro 2000 basi wote wangesema Raul.

Cha kushangaza ni kwamba ni kwamba Gwiji huyu wa Real Madrid alipiga Penati yake juu kabisa ya Goli la Fabien Barthez alipopewa nafasi hiyo, mechi hii iliisha kwa ushindi wa Ufaransa na timu hiyo iliweza kufanikiwa kutwaa kombe hilo baada ya kuifunga Italia fainali nchini Uholanzi

ZICO

penati 5

Inaaminika na Mashabiki wengi sana wa mpira kwamba timu ya Brazil ya mwaka 1986 ndio timu bora zaidi ambayo haikuweza kutwaa taji la Kombe la dunia.Ila mambo yangeweza kuwa tofauti sana laiti Zico angeweza kufunga mkwaju wake wa Penati kwenye mechi iliokuwa na msisimko sana kati ya Brazil na Ufaransa kwenye hatua ya robo fainali ya kombe la Dunia la mwaka huo.

Zico alitokea Benchi kwenye mechi hii na dakika chache baadae alifanikiwa kuipatia timu yake Penati ambayo yeye mwenyewe alikabidhiwa kuipiga.Zico alipiga penati yake katikati ya mikono ya golikipa wa Ufaransa Joel Bats ndani ya jua kali sana huko nchini Mexico.Ufaransa waliweza kuifunga Brazil kwa mikwaju ya Penati na kuendelea mbele kwenye kombe hilo.

LIONEL MESSI

penati 6

Chelsea ailkuwa amebaki na wachezaji 10 uwanjani katika mechi ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya kati yao na Barcelona mwaka 2012, na swali lililokuwa limebaki lilikuwa ni mda gani tu ambao Barcelona wangeweza kupata goli muhimu la tatu ambalo lingewawezesha kununua tiketi yao ya kwenda kucheza fainali ya ligi ya mwaka huo dhidi ya Bayern Munich uwanjani Allienz Arena.Na kama kweli vile Barcelona walibahatika kupata Penati na Lionel Messi akapewa majukumu ya kupiga Penati hiyo.Messi alipiga Penati yake mwambani.

Chelsea walipaki basi lao vizuri kabisa na wakafinikiwa kutinga fainali ya mwaka huo ambapo wakafanya maajabu tena kwa kumfunga Bayern Munich kwa mikwaju ya Penati na kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza.

ARJEN ROBBEN

penati 7

Ama kweli mwaka wa 2012 Chelsea walikuwa na Bahati ya Ajabu, katika fainali ya ligi ya mabingwa ya mwaka huo Drogba alifanikiwa kurudisha Goli la Bayern Munich dakika ya 90 ya mchezo huo na kama ilikuwa haitoshi  ndani ya dakika za nyongeza mpiga Penati wa Bayern Munich Arjen Robben alikosa Penati ya Bayern Munich ambayo ingeweza kumaliza mchezo huo kabisa.

Kitendo hichi killipa nguvu mpya Chelsea kwani waliweza kumfunga Bayern kwa mikwaju ya Penati ndani ya uwanja wa Bayern Munich Allianz Arena.

DAVID BECKHAM

Inaonekana kwamba timu ya Uingereza ina mkosi na Penati maana mara nyingi hutolewa kwa sababu ya Penati kwenye Michuano karibia yote wanayoshiriki.Katika Euro ya 2004 kapteni wa Uingereza David Beckham alijitokeza kuchukua jukumu lake kama mpiga penati wa timu hiyo pale Uingereza ilipopata Penati dhidi ya Ureno kwenye hatua ya Robo fainali ya Kombe hilo.Beckham  alipaisha Penati yake na mechi ikaisha 2-2 baada ya dakika 120 za mchezo.Ureno ilifanikiwa kuitoa Uingereza kwa mikwaju ya Penati 6-5 huku waingereza wengi wakibaki kutoelewa kwanini timu yao haiwezi kushinda Penati.

ANDRIY SHEVCHENKO

penati 8

Fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 2005 ilikuwa ya ajabu sana, Liverpool waliweza kurudi kutoka kuongozwa  kwa goli 3-0 halftime mpaka 3-3.Andriy Shevchenko alikuwa mshambuliaji bora zaidi duniani kwa wakati huo na iliwashangaza wengi sana pale alipochezea nafasi nzuri sana ya kuirudisha timu yake mbele tena kwenye mechi hiyo kwani kipa wa Liverpool Jerzy Dudek aliweza kudaka shuti lake kimaajabu.Mechi hii ilishindwa kuzaa goli lingine na hatimaye ikaenda mikwaju ya Penati

Inaonekana Shevchenko alikuwa bado anawazia nafasi ile aliokosa, kwani ilipofika zamu yake kupiga mkwaju wake, alipiga Penati mbovu sana na kuiwezesha timu ya Liverpool kutwaa Kombe la ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tano.

JOHN TERRY

penati 9

Fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya mwaka 2008 kati ya Chelsea na Man United ilikuwa kama filamu iliyoandikwa kwa ajili ya John Terry.

Huku mashabiki wake wakimtazama John Terry Kapteni wa klabu ya Chelsea na kipenzi cha mashabiki wa Chelsea aliyechezea klabu  hiyo tokea  Utotoni, alipewa Penati ya Mwisho ambayo kama angeifunga ingeipa Chelsea kombe lao la kwanza la ligi ya mabingwa Ulaya ambalo walikuwa wanalitamani sana.

Katika moja ya matukio ambayo shabiki yeyote wa mpira hatokuja kulisahau John Terry aliteleza kwenye Uwanja wa Moscow uliokua umelowa kwa sababu ya mvua nzito na kupiga Penati yake mwamba wa kulia wa goli la Van der Sar.Man United walifanikiwa kutwaa kombe hilo huku John Terry akibaki akitiririkwa na machozi.

ROBERTO BAGGIO

penati 10

Hii ndiyo Penati inayokumbukwa na mashabiki wengi sana dunia nzima, katika kombe la Dunia la kwanza kabisa kuamuliwa na mikwaju ya Penati mwaka 1994 nchini Marekani, tegemezi wa timu ya Italia Roberto Baggio aliyekuwa  mchezaji bora kwenye michuano ya mwaka huo, alipewa Penati ya mwisho ambayo ingeamua mshindi wa kombe hilo, Baggio aligeuka kutoka kuwa kipenzi cha Mashabiki mpaka adui pale alipopiga Penati yake nje kabisa ya Goli na kuwawezesha Brazil kuwa mabingwa wa Dunia kwa mara ya nne.

ASAMOAH GYAN

penati 11

Hii ndiye Penati ilioumiza Roho za Waafrika wote kwa Ujumla.Katika mechi ya Robo fainali ya Kombe la Dunia 2010 lililofanyika kwa mara ya kwanza barani  Afrika, timu ya taifa ya Ghana ama the Black Stars ikiongozwa na mshambuliji wao Asamoah Gyan ilikutana na team ya Uruguay nayo ikiongozwa na mshambuliaji wao Mahiri Luis Suarez.

Team ya Ghana iliweza kuteka dunia kwa mpira wao wa kasi na wa kuvutia na ilikuwa ikiwania kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika nusu fainali ya kombe hilo.Mechi hii ilikuwa 1-1 mpaka dakika ya 90 pale ambapo timu ya Ghana ilizawadiwa Penati baada ya mshambuliaji Luis Suarez kuzuia mpira kwa maksudi kabisa na mikono golini yani kama vile yeye ndiye aliyekuwa kipa.Waafrika wote walitazama bila kuamini Pale Nyota wa Ghana Asamoah Gyan alipopiga mwamba na Penati  yake akiacha watu wote wakisitika.Mechi ilienda adi mikwaju ya Penati na japo Gyan aliweza kufunga Mkwaju wake timu ya Uruguay ilishinda mikwaju hiyo ya Penati huku wakivunja roho za mashabiki wa mpira Dunia nzima.penati



Comments