URUGUAY, JAMAIKA ZACHEZEA KICHAPO COPA AMERIKA



URUGUAY, JAMAIKA ZACHEZEA KICHAPO COPA AMERIKA
Na Dac Popos, Globu ya Jamii. 
Michuano ya Copa Amerika imeingia katika siku yake ya tatu kwa michezo miwili kupigwa katika viwanja tofauti huko nchini Marekani. 

Mtanange uliotolewa macho na masikio na wengi ulikuwa kati Uruguay ya Luis Suarez na Mexico ya Javier Hernandez 'chicharito'. Twaweza sema kuwa Uruguay walifungwa kabla ya mpira kuanza, kwa sababu mbili, ya kwanza ni kukosekana kwa mshambuliaji wa hatari Luis Suarez aliye majeruhi na pili kutopigiwa wimbo wao wa taifa na badala yake wakapigiwa wimbo wa taifa wa Peru.

Mchezo ulianza kwa kasi na dakika ya nne tu mlinzi wa Uruguay Max Perreira alijifunga mwenyewe kwa kichwa katika harakati za kuokoa, hadi mapumziko Mexico 1 Uruguay 0. Kipindi cha pili Uruguay walijitahidi kubadili mchezo na kunako dakika ya 74 Diego Godin akaisawazishia timu yake bao. Mexico wakaja juu tena na kijipatia mabao mawili ndani ya dakika tano, kwani dakika ya 85 R.Marquez alifunga goli la pili na dakika ya 90 Hector Herrera akagongelea msumali wa mwisho.
Mtanange mwingine uliwakutanisha 'Reggae Booys' Jamaica waliokipiga na Venezuela, ambapo Venezuela walifanikiwa kuondoka na pointi zote tatu kwa kuifunga Jamaica goli 1-0. Goli hilo liliwekwa kimiani na mshambulizi Josef Martinez, huku mchezaji Rodoph Austin wa Jamaica akilambwa kadi nyekundu. Pia kocha wa timu hiyo Juan Carlos Osorio alitolewa uwanjani na kwenda kukaa jukwaani kutokana na kumtolea maneno makali mwamuzi.

Hadi kipyenga cha mwisho kuashiria mchezo umemalizika, Venezuela1 Jamaica 0.

Leo tunahitimisha mechi za mzunguko wa kwanza ambapo ni kati ya
BOLIVIA vs PANAMA
ARGENTINA vs CHILE

Pia hapo baadaye usikose kupitia ukurasa huu kwa sababu rasmi tunaanza kukuletea dondoo mbali mbali za kuelekea UFARANSA kwenye patashika ya EURO 2016.


Comments