Uhuru Selemani ni jina kubwa kwenye soka la Tanzania, kwa sasa anacheza timu ya Royal Eagles inayoshiriki ligi daraja la kwanza Afrika Kusini ikiwania kupanda kucheza ligi kuu ya nchini humo maarufu kama PSL.
Jamaa kwa sasa yupo nchini kwa mapumziko. Akiwa Bongo ameamua kujiunga na timu ya Temeke Market inayoshiriki michuano ya Sport Extra Ndondo Cup 2016.
Shaffihdauda.com ilimtafuta Uhuru mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa ufunguzi kati ya mabingwa watetezi Faru Jeuri vs Temeke Market na kuzungumza naye mambo kadhaa kuhusu soka la Bongo na hata huku 'Sauz' ambako anacheza soka la kulipwa.
Shaffihdauda.co.tz: Uhuru unayaonaje mashindano ya Ndondo Cup?
Uhuru: Ni mashindano mazuri sana kwasababu yanatoa nafasi kwa wachezaji ambao hawana timu kupata muda wa kucheza mechi na kuonesha uwezo wao na kutoka hapo wanaweza kusajiliwa na vilabu vingine vya ligi daraja na pili, ligi daraja la kwanza na hata ligi kuu.
Pia michuano hii inatupa nafasi sisi wachezaji wa ligi kupata muda wa kucheza kipindi cha likizo na kujiweka fiti muda wote na si kukaa nyumbani tu hadi ligi ianze tena.
Shaffihdauda.com: Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiwaponda wachezaji wenye majina makubwa ambao wanakuja kucheza mechi za Ndondo Cup, kuna ubaya wowote mchezaji mwenye jina au anayetokea klabu kubwa kucheza Ndondo?
Uhuru: Wanakosea sana, kwahiyo wanataka tukae nyumbani kipindi chote cha likizo? Kwasababu ligi zinaposimama, wachezaji wote wanapewa likizo hadi pale watakapoitwa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi. Sisi tunapokuja kucheza huku haina maana kwamba tuna njaa na tunaka hela. Tunakuja kucheza ili kuboresha viwango vyetu, lakini tunakuja kuwapa hamasa wachezaji wa huku ili nao watafute mafanikio tuliyonayo sisi.
Hata kama Ndondo isingekuwepo bado ningeenda kwenye timu ya mtaani kwangu na kuomba kufanya nao mazoezi, kwahiyo kucheza huku si kujishusha, mbona huku ndiko tulikotoka hadi tukafika huko tulipo?
Shaffihdauda.com: Unaonaje uwezo na vipaji vinavyooneshwa na wachezaji wa michuano ya Ndondo?
Uhuru: Kuna wachezaji wanauwezo mkubwa sana huku na vipaji vya hali ya juu, ndiyo maana tunasema kupitia mashindano haya wapo watakaoonekana na kusonga mbele zaidi. Itakuwa vizuri kama makocha wa timu mbalimbali watayatilia maanani mashindano haya na kutafuta wachezaji kwa ajili ya timu zao hasa kipindi hiki cha usajili.
Comments
Post a Comment