NYOTA wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Roberto Carlos amempa mbinu straika Cristiano Ronaldo akisema kwamba anatakiwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya fainali za mataifa ya Ulaya "Euro 2016" ili aweze kutawazwa tena kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Ballon d'Ol.
Beki huyo alisema juzi kwamba anavyoamini straika huyo wa timu ya taifa ya Ureno ndie atakayekuwa tishio katika fainali hizo zitakazoanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki hii nchini Ufaransa hata kama hataiwezesha timu yake kutwaa ubingwa.
"Cristiano Ronaldo atatwaa tuzo ya Ballon d'Ol hata kama hatafanikiwa kutwaa ubingwa wa euro," alisema mara baada ya mechi ya Corazon Classic ambayo huwakutanisha wachezaji wa zamani, iliyopigwa juzi kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.
Mbali na hilo, Carlos mwenye umri wa miaka 43 pia alimtabiria Ronaldo kutwaa tena taji la mchezaji bora la dunia la Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA), Ballon d'Ol ambalo kwa sasa linashikiriwa na nyota wa Barcelona, Lionel Messi baada ya kuipa ubingwa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Katika mchezo huo uliopigwa mwishoni mwa mwezi uliopita katika uwanja wa San Siro mjini Milan, staa huyo mwenye umri wa miaka 31 ndie aliyepiga penati ya mwisho baada ya Real Madrid kwenda sare ya bao 1-1 na mahasimu wao, Atletico Madrid katika muda wa kawaida na wa nyongeza.
"Messi ni mchezaji mzuri lakini kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa kunakuongezea sifa nyingi," alisema Carlos.
"Mchezaji bora wa dunia huwa anaamuliwa na mashindano. Nafikiri atakuwa bora tena duniani," alisema staa huyo wa zamani."
Comments
Post a Comment