KOCHA wa timu ya taifa ya Panama, Heman Gomez amemshauri straika wa Real Madrid, James Rodriguez kwamba ni lazima akubali kuwa hataweza kupata nafasi ya kucheza chini ya Zinedine Zidane na hivyo aachane na timu hiyo.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 24 aliyeripotiwa kusajiliwa kwa euro mil 80 mwaka 2014 akitokea FC Monaco lakini kwa sasa anakosa nafasi ya kucheza tangu Januari alipoteuliwa Zidane kuwa kocha mkuu wa timu hiyo ya mjini Madrid.
Katika kipindi cha misimu kadhaa iliyopita, James alikuwa akihusishwa kuondoka kwenye klabu hiyo ya Santiago Bernabeu na huku Manchester United ikiwa miongoni mwa klabu zilizokuwa zikimwinda licha ya mwezi uliopita kusema kuwa atahakikisha anapigania nafasi yake.
Hata hivyo kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Colombia ambaye kwa sasa anainoa Panama na ambaye amewahi kumfundisha James katika mwaka 2010 na 2011, alisema kuwa sio jambo zuri kuona mchezaji wa timu ya taifa akikubali kusugua benchi.
"Nitajaribu kumpa ushauri James," Gomez aliuambia mtandao wa WIN Sports. "Ni vizuri kwake kwenda katika timu nyingine kwa sababu inaonekana kocha wake hataki kumchezesha."
Comments
Post a Comment