NI kama vile Zlatan Ibrahimovic amewapiga chenga ya mwili mashabiki wa Manchester United baada ya kuueleza ulimwengu kuwa bado watalazimika kuvuta subira kabla hajaitaja timu yake mpya.
Siku ya Jumanne, Zlatan Ibrahimovic aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Paris ambao lengo lake kuu ilikuwa ni kutambulisha biashara yake mpya ya mavazi, lebo inayokwenda kwa jina la A-Z, lakini pia katika mkutano huo alitarajiwa kutaja timu atakayojiunga nayo.
Manchester United ndiyo klabu inayohusishwa zaidi na usajili wa Ibrahimovic na dunia nzima ilitarajia kuwa jambo hilo lingewekwa wazi jana.
Lakini badala yake mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden akaishia kuitangaza A-Z na kusema hatma yake ya soka itajulikana baadae.
"Bado hakuna uthibitisho," alisema Ibrahimovic pale alipoulizwa kuhusu Old Trafford. "Hakuna ninachoweza kusema ndiyo. Mnapaswa kuwa na subira.
"Napenda kuendelea kuwaacha mkijiuliza wapi nitakapoelekea na nitapochoshwa na hizi stori basi nitawaeleza klabu nitakayojiunga nayo.
"Hatma yangu ni A-Z (lebo yake mpya), ifuatilie A-Z na utajua hatma yangu. Manchester pia watavaa A-Z, msijali itafika mpaka huko pia," alisema Ibrahimovic.
Zlatan Ibrahimovic akitambulisha A-Z lebo yake mpya ya biashara yake ya mavazi
Manchester United wanapaswa kuendelea kuvuta subira kabla Zlatan Ibrahimovic hajataja timu yake mpya
Comments
Post a Comment