BEKI mkongwe Patrice Evra amesema kuwa walikuwa wakifahamu fika kuwa watakutana na ushindani mkali wakati watakapoikabili Jamhuri ya Ireland katika mechi ya hatua ya 16 Bora ya michuano ya fainali za Mataifa ya Ulaya "Euro 2016".
Katika mchezo huo wa juzi uliopigwa mjini Lyon, wenyeji hao walijikuta wakiwa nyuma dakika ya pili kwa bao la penati lililofungwa na staa Robbie Brady kabla ya kuzinduka na kupata ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na straika wao, Antoine Griezmann.
Na wakati Ufaransa wakionekana kama ingefungwa kutokana na kiwango ilichoonyesha Ireland kipindi cha kwanza, beki huyo wa zamani wa Man United anadai kuwa walikuwa wakifahamu wangekutana na jambo kama hilo.
"Ilikuwa ni mechi ngumu lakini tulikuwa tukilifahamu hilo," Mfaransa huyo alikiambia kituo kimoja cha televisheni.
"Hakuna asiyekutana na mechi ngumu katika mashindano, mfano ni kama usiku uliopita watu walikuwa wakisema Croatia watapata ushindi kirahisi dhidi ya Ureno, lakini niwe mkweli nilikuwa nikifahamu leo itakuwa ni mechi ngumu," aliongeza staa huyo.
Comments
Post a Comment