BEKI wa kati wa timu ya AS Monaco na timu ya taifa ya Ureno, Ricardo Carvalho amemtaka kocha Jose Mourinho kufuata nyayo za kocha wa zamani, Alex Ferguson kwa kushinda mataji mengi akiwa na Manchester United.
Mourinho amefanikiwa kurejea katika michuano ya Ligi Kuu England akiwa na Man United baada ya kuchukua nafasi ya kocha wa zamani wa timu hiyo, Louis Van Gaal kwa mkataba wa miaka mitatu.
Akiwa na nafasi ya kuonyesha uwezo wake akiwa na klabu hiyo ya Old Trafford, baada ya kufukuzwa na Chelsea kutokana na kushindwa kuiwezesha kutetea ubingwa wake, Carvalho ambaye amewahi kucheza chini ya Mourinho wakiwa Stanford Bridge na Real Madrid, anasema kuwa ana uhakika ataiwezesha Man United kutwaa taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2012/13.
"Nafahamu fika Jose anaweza kupata mafanikio akiwa Manchester United," alisema Carvalho ambaye anajiandaa na michuano ya fainali za Mataifa ya Ulaya "Euro 2016" akiwana timu ya taifa ya Ureno.
"Sina wasiwasi na hilo la kwamba anaweza kurejesha mataji tena Man United na ambayo yatawafanya kuwa mabingwa," aliongeza Mreno huyo.
Alisema, japokuwa anafahamu kama itakuwa ni katika mwaka wake wa kwanza, wa pili ama wa tatu, lakini ni kwamba ana uhakika atatwaa ubingwa na akasema kuwa kwa utabiri wake itakuwa ni katika mwaka wake wa pili.
Comments
Post a Comment