WAZIRI MKUU wa Italia, Matteo Renzi,            amempongeza Claudio Ranieri (pichani juu) baada ya kushinda            taji la Premier League akiwa na Leicester City Jumatatu usiku.
        Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Renzi            aliandika kuwa "mafanikio makubwa zaidi katika historia ya            soka la England yameongozwa na Mtaliano", huku akimpongeza            Ranieri na klabu yake ya Leicester City kwa kushinda taji            hilo.
        Ranieri, 64, amekuwa gumzo katika dunia ya            michezo kwa mafanikio yake, akiiongoza Leicester kubeba            ubingwa huku wakiwa na mechi mbili mkononi kufuatia Tottenham            Hotspur kutoka sare ya 2-2 nyumbani kwa Chelsea.
        Ranieri alikabidhiwa mikoba King Power            Stadium kiangazi kilichopita baada ya Foxes kuweza kuepuka            kushuka daraja karibu na mwisho wa msimu uliopita.
        Licha ya kampuni za kamari kuipa Leisester            5,000-1 kuweza kuibuka bingwa mwanzo wa msimu, Ranieri            amewaonyesha kuwa walikuwa wakifikiri sivyo, na kujizolea sifa            kutoka kila kona na kupata heshima kubwa nyumbani kwao Italia.
        
Comments
Post a Comment