MISHAHARA YALETA BALAA MSIMBAZI …WACHEZAJI SIMBA WAGOMEA SAFARI YA SONGEA



MISHAHARA YALETA BALAA MSIMBAZI …WACHEZAJI SIMBA WAGOMEA SAFARI YA SONGEA

WACHEZAJI wa kigeni wa klabu ya Simba, pamoja na mchezaji mzawa Mwinyi Kazimoto, wameikacha safari ya klabu hiyo iliyokuwa ikienda mkoani Ruvuma kuvaana na Majimaji ya Songea.

Wachezaji waliokacha safari hiyo ni Vincent Angban, Juuko Murshid, Emery Nimubona, Justice Majabvi, Hamis Kiiza, Brian Majwega na Mwinyi Kazimoto.

Chanzo kikuu cha wachezaji hao kukacha safari hiyo iliyofanyika leo kwa ajili ya mchezo wao wa 28 wa Ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Majimaji ya Songea, ni kutolipwa mishahara yao.

Ofisa habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, alisema kuwa sababu ya kuchelewa kuwapa mishahara wachezaji wao inatokana na wadhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuchelewa pia kuwapatia fedha za udhamini.

 "Mfano Mwinyi alikuwa hapatikani kabisa kwenye simu, lakini hawa wengine walikataa kwenda sababu ya kutolipwa mishahara yao"alisema Manara.

Licha ya kutaja wachezaji hao, kuna wachezaji ambao wameshindwa kwenda Songea kutokana na kuwa wagonjwa, ambao ni Raphael Kiongera, Jonas Mkude, Awadhi Juma na Ibrahim Ajib ambaye alionyeshwa kadi nyekundu Jumapili katika mechi ya ligi dhidi ya Mwadui FC


Comments