HUU ni ushauri tu ambao ni juu ya wenyewe, Manchester United kuukubali ama kuupotezea.
Katika kinachoaminika kutaka kuona United ikirejea katika kiwango chake cha zamani, Mashetani Wekundu hao wameshauriwa kumsajili kiungo wa Leicester City, Danny Drinkwater.
Ushauri huu umetolewa na aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Manchester United, Rene Meulensteen.
Kwa mujibu wa Meulensteen, kiungo huyo wa Mabingwa wa premier msimu huu, Leicester City amewahi kupita Old Trafford kama mchezaji kinda ambaye kwa sasa ni kati ya wachezaji wanaoweza kuirejesha katika uimara United katika msimu ujao.
Kocha huyo alisema kuwa, United wamekosa wachezaji wa aina ya Drinkwater ambao wakipatikana na wengine, watairudisha timu katika mazingira ya kuwa tishio kama ilivyo enzi ya kocha Alex Ferguson.
"Kama ukitaka kuichambua Leicester City na sababu iliyochangia kutwaa ubingwa, huwezi kukosa kutaja kuimarika kwa idara yao ya kiungo iliyoongozwa vyema na Drinkwater."
"Kwangu mimi kama kocha, ninaamini kiungo huyo alikuwa ndie bora na aliyechangia ubingwa wa The Fox na kwamba United wanaweza kuimarisha kikosi cha msimu ujao kwa kumnyakua," alisisitiza Meulensteen.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 ni zao la United kwani ametokana na mradi wa kulea na kuibua vipaji ndani ya Old Trafford lakini alishindwa kupata mafanikio na kuamua kutimkia Leicester City mnamo Januari, 2012.
Tangu hapo Drinkwater amekuwa katika uhakika wa kutumika katika kikosi cha kwanza cha mbweha hao wa King Power na hadi msimu huu alipong'ara na kuipa ubingwa.
Kiwango chake cha msimu huu kimemuwezesha pia kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England kitakachoshirika michuano ya mataifa ya Ulaya itakayofanyika nchini Ujerumani.
Meulensteen bado anasisitiza kuwa United wana nafasi ya kumrejesha Drinkwater katika viunga vya Old Trafford na kuwa msaada wa timu msimu ujao.
"Drinkwater bado ana historia ndani ya Manchester United kwasababu ni zao lao na wakati wa kufanya hivyo ni sasa."
"Wakati mwingine lazima klabu iangalie wapi ilipokosea na kutafuta njia ya kujiimarisha, kipindi hiki sio cha kuangalia zaidi wachezaji wa kigeni kwasababu wanahitaji muda mwingi wa kujiweka sawa."
Comments
Post a Comment