LIVERPOOL YATHIBITISHA INAMTAKA MATS HUMMELS WA DORTMUND



LIVERPOOL YATHIBITISHA INAMTAKA MATS HUMMELS WA DORTMUND
KLABU ya Liverpool imeingia katika vita ya kumwania beki mahiri wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, Mats Hummels.

Habari zinasema kwamba kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameamua kuingia katika vita ya kumwania beki huyo kutokana na ukweli kwamba beki huyo sasa hana mapenzi tena ya kucheza katika klabu hiyo ya zamani ya mwalimu huyo.

Klopp amekaririwa akisema kwamba anataka kumsajili beki huyo kutokana na mahitaji ya sasa ya beki wa aina yake na kwamba haoni kama ni lazima beki huyo kwenda katika timu pinzani ya Bayern Munich.

"Ni kweli kwamba mchezaji huyo ameonekana anataka kwenda Bayern lakini mimi pia nataka kuzungumza nae na kumsajili hapa Liverpool," amesema Klopp.

Mapema wiki iliyopita beki huyo ameiambia klabu yake kuwa anataka kujiunga na viongozi wa Ligi ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga, Bayern Munich baada ya kukamilika msimu huu.

Mats Hummels amesema hana amani katika kikosi hicho na kwamba anataka kukatiza mkataba na kuangalia maisha mengine.

Mapema wiki hii, mwenyekiti wa Bayern, Karl Heinz Rummenigge alifichua kuwa klabu hiyo ilikuwa tayari inafanya mazungumzo na nahodha huyo wa Dortimund kuhusu uhamisho.

Dortmund imethibitisha katika taarifa kuwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 27 ambaye ana mkataba hadi Juni, 2017 amewasilisha ombi rasmi la kutaka kuondoka.

Kwa sasa Bayern haijatoa ofa na kuwa mchezaji huyo ataweza kuondoka tu ikiwa kwa kutolewa kiasi cha pesa kitakachokubaliwa.

Hummels atajiunga na Mario Goetze aliyeondoka mwaka 2013 kwa kiasi cha euro milioni 37 na mshambuliaji Robert Lewandoswki aliyesaini mwaka 2014.

Hata hivyo, kocha wa Liverpool amesema ni wakati mwafaka sasa kumsajili mchezaji huyo aisema kwamba yuko katika orodha ya wachezaji ambao anawataka kutoka Borussia alikotokea kabla ya kujiunga na Liverpool.


Comments