LIVERPOOL YASAKA KIPA MPYA ...Jurgen Klopp ampigia hesabu Loris Karius wa Mainz



LIVERPOOL YASAKA KIPA MPYA ...Jurgen Klopp ampigia hesabu Loris Karius wa Mainz

KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp ni kama ameona umuhimu wa kuongeza nguvu katika idara ya ulinzi, upande wa mlinda mlango.

Katika azma hiyo ameweka nguvu katika kumwania mlinda mlango kinda anayekipiga katika kikosi cha timu ya Mainz, Loris Karius.

Mlinda mlango huyo ambaye pia ni kati ya wanandinga wanaounda timu ya taifa ya vijana ya Ujerumani, ameingia katika rada za Klopp kwa ajili ya usajili wa majira ya kiangazi.

Klopp ameweka mezani dau la pauni 8 mil kwa ajili ya kumuita ndani ya kikosi cha Majogoo wa jiji la Liverpool.

Loris Karius mwenye umri wa miaka 22, amekuwa katika kiwango cha uimara wa kumshawishi bosi huyo wa Anfield.

Mlinda mlango huyo ameitumikia Mainz katika michezo tisini hadi sasa na kufanya vizuri katika mechi 27 ambazo hakuweza kuruhusu nyavu zitikisike.

Amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha timu ya vijana na ametajwa katika orodha ya walinda mlango bora nchini Ujerumani na sifa hizo ndio zilizomfanya Klopp kumtupia jicho tangu akiwa Borrusia Dortmund.

Hatua ya Klopp imelenga kuongeza ushindani wa namba kikosini, hususan kwa mlinda mlango wa sasa, Simon Mignolet.

Hata hivyo taarifa za ndani zimesema kuwa, Klopp yumo katika harakati za kutaka kuachana na mlinda mlango Adam Bogdan ambaye ameshindwa kuonyesha kiwango cha kuridhisha.


Comments