DALEY BLIND AMLILIA MHOLANZI MWENZAKE LOUIS VAN GAAL... asema alistahili kupewa muda zaidi Old Trafford
DALEY Blind amesema amefadhaishwa na kutimuliwa kazi kwa Louis Van Gaal akiona kwamba kocha huyo Mholanzi mwenzake hakupewa muda wa kutosha madarakani Manchester United.
Van Gaal alitimuliwa Jumatatu hii, siku mbili tu baada ya kuiongoza klabu hiyo kutwaa taji la kwanza, Kombe la FA, tangu utawala wa Sir Alex Ferguson ulipomalizika mwaka 2013.
Blind alisajiliwa na Van Gaal Manchester United kwa ada ya uhamisho wa pauni mil 14 akitokea Ajax mwaka 2014 na anaamini kwamba Mholanzi mwenzake alistahili kupewa muda zaidi wa kuweka mawazo yake Old Trafford.
"Daima nimekuwa nikifanya kazi vyema nae na natamani ushirikiano huu ungeendelea kwa muda mrefu zaidi," Blind aliwaambia waandishi wa habari katika kambi ya timu ya taifa ya Uholanzi nchini Ureno.
"Kocha katika klabu kubwa kama England, ni kawaida kuwa katika presha, lakini katika kipindi cha miezi sita iliyopita hakuwa akitendewa haki. Nadhani makocha kama Louis Van Gaal ambao wameshinda mataji mengi, wanastahili kuheshimiwa zaidi."
Comments
Post a Comment