CHELSEA imeizidi ujanja Manchester United katika mauzo ya jezi miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England msimu wa 2015/16, huku ikishika nafasi ya tatu duniani, licha ya kusuasua na kushindwa kjutetea ubingwa.
Mauzo ya jezi za Chelsea yamepanda kwa asilimia 39 kutoka msimu uliopita na kufikia jezi 3,102,000, ikiwa ni asilimia tano zaidi ya mauzo ya United iliyofanikiwa kuuza jezi 2,977,000.
Arsenal imeimarika nafasi ya tatu kwa klabu za England na ya saba duniani ikiuza jezi 2,055,000.
Kwa mujibu wa wakala wa masoko wa vifaa vya michezo, Euroamericas, Barcelona ndio kinara barani Ulaya ikiuza jezi 3,637,000 ikifuatiwa na Bayern Munich iliyouza jezi 3,312,000.
Kuendelea kufanya vizuri kwa Atletico Madrid iliyofanikiwa kuingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu kumeifanya kuingia 10 bora kwa mara ya kwanza kwa kuuza jezi 1,977,000 idadi ambayo imeiwezesha kushika nafasi ya nane.
Orodha kamili ya vinara wa kuuza jezi ni Barcelona (1), Bayern Munich (2), Chelsea (3), Manchester United (4), Real Madrid (5), PSG (6), Arsenal (7), Atletico Madrid (8), Juventus (9), na AC Milan (10).
Comments
Post a Comment