Licha ya kushinda 2-1, lakini Bayern Munich imetolewa na Atletico Madrid katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Atletico Madrid ambayo ilishinda 1-0 nyumbani kwao katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumatano iliyopita, imesonga mbele kwa faida ya goli la ugenini na sasa inasubiri mshindi wa Jumatano usiku kati ya Manchester City na Real Madrid.
Bayern ambayo hii inakuwa ni mara ya tatu mfululizo kutolewa katika nusu fainali, ilipata bao la kuongoza dakika ya 31 kupitia kwa Xabi Alonso.
Dakika tatu baadae, miamba hiyo ya Ujerumani ikapoteza nafasi ya kutanua uongozi wao baada ya mshambuliaji Thomas Mueller kukosa penalti dakika ya 34.
Antoine Griezmann akaisawazishia Atletico 54, lakini Robert Lewandowski akafufua matumaini ya Bayern Munich kwa kuifungia bao la pili dakika ya 74.
Zikiwa zimesalia dakika 6 mpira kumalizika, Atletico Madrid wakapoteza penalti iliyopigwa na Fernando Torres.
Comments
Post a Comment