BASTIAN SCHWEINSTEIGER WA MAN U AGEUKIA FILAMU



BASTIAN SCHWEINSTEIGER WA MAN U AGEUKIA FILAMU
MAISHA ni popote, ukona upande mmoja umebana, unageukia upande mwingine ilimradi maisha yasonge mbele.

Ndivyo unavyoweza kusema baada ya nyota mmoja katika kikosi cha Manchester United ambaye anaandamwa na majeruhi, sasa ameamua kuanza maisha mapya wakati akiendelea kujiuguza.

Habari zinasema kwamba nyota huyo Bastian Schweinsteiger anajiandaa kucheza tangazo jipya la iPhone app, Clash of Kings.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani akiwa na kikosi cha Old Trafford ndani ya msimu wake wa kwanza kwenye premier league hajafurahia maisha yake mapya kwenye Ligi hiyo kutokana na kuandamwa na majeruhi ya mara kwamara huku kukiwa na taarifa huenda akaikosa michuano ya euro 2016 itakayoanza mwezi Juni nchini Ufaransa.

Kiungo huyo mwenye miaka 31, anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwamuda mrefu zaidi katika maisha yake ya soka na muda huo atautumia kutengeneza tangazo jipya la Clash of Kings.

Kwa mujibu wa gazeti la Bild la nchini Ujerumani, Schweinsteiger atacheza kama mfalme kwenye tangazo hilo la kibiashara huku akiwataka watu waunganishe program hiyo ya gemu na kucheza. 

Bado haijawekwa wazi kwamba ni lini tangazo hilo litaachiwa, lakini litakuwa linavutia kumuona Schweinsteiger kwenye sehemu ya tangazo hilo.


Mchezaji huyo ni kama anafuata nyayo za mchezaji wa zamani wa Manchester United, Eric Cantona kuamua kucheza muvi baada ya kutundika daruga.


Comments