ARSENE WENGER AENDELEA KUOTA KUMSAJILI LIONEL MESSI


ARSENE WENGER AENDELEA KUOTA KUMSAJILI LIONEL MESSI
INGAWA inawezekana kuwa ni ndoto za alinacha, lakini bado bosi wa Washika Mitutu wa jiji la London, Arsene Wenger anaamini kukamilika kwa ndoto aliyoanza miaka mingi nyuma ya kumnasa Lionel Messi.

Ndoto za Mfaransa huyo zimekuja siku chache baada ya kubainisha azma ya kumwita kundini nyota huyo raia wa argentina. Katika mpango wake wa miaka mitano nyuma, Wenger alikuwa akimfukuzia nyota huyo wa Barcelona ingawa mpango wake huo ulizimwa bila ya mafanikio.

Lakini hata sasa Wenger amekiri kuvutiwa na mpachika mabao huyo mwenye heshima na hadhi kubwa kwa sasa ulimwenguni kote.

Katika kunukuliwa kwake, bosi huyo alisema alijaribu kumsajili Lionel Messi kama mpango wa kutaka kuwanyakua wachezaji watatu wachanga wa klabu hiyo.

Messi alikuwa na miaka 15 wakati huo na mwenzake Gerrad Pique pamoja na aliyekuwa kiungo wa kati wa Arsenal, Cess Fabregas.

Wenger: "Tulitaka kumchukua Fabregas, Messi na Pique lakini tukafanikiwa kumpata Fabregas pekee."
Wenger aliongeza: "Nadhani Messi mwenyewe hakutaka kujiunga nasi."

Fabregas alichezea klabu ya Arsenal kwa miaka minane kabla ya kurudi Barcelona, huku Pique akijiunga na Manchester United mwaka 2004.

Messi mwenye umri wa miaka 27, amechezea timu ya Barcelona kwa muda wote na kuisaidia kushinda mataji sita ya La Liga pamoja na Kombe la Klabu Bingwa mara tatu baada ya mpango wa kujiunga na Arsenal kugonga mwamba.

Hata hivyo Wenger amepinga madai kwamba mpango huo ulifeli kutokana na matatizo ya Messi na familia yake.

"Messi ni mchezaji mkubwa nakubali kuhusu ukweli huu, lakini Arsenal nayo ni klabu kubwa ambayo ina uwezo wa kumsajili mchezaji huyu."

"Nimekuwa na ndoto hii tangu zamani na hata sasa, ninaamini kuwa uwezo na sababu hii bado ninayo na hata mipango ya awali niliyoanza ninaweza kuiendeleza katika muda muafaka."

"Muda unaweza kufikia ni jambo la kusubiri na kuvuta subira. Isiwe msimu ujao lakini mwisho wa siku kuna jambo linaweza kutokea kuhusiana na hatua yangu hii ya kuwa na nyota mkubwa, bila shaka anaweza kuwa Lionel Messi," amenukuliwa Wenger.


Huenda taarifa hizi zinakuja katika siku hizi ambazo kikosi cha Arsenal kimejizatiti katika kuhakikisha kinakuwa na matokeo mazuri ifikapo mwisho wa msimu huu ingawa wamepoteza mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita.


Comments