ZIDANE AWEKA WAZI KUWA CRISTIANO RONALDO NI "UNTOUCHABLE"



ZIDANE AWEKA WAZI KUWA CRISTIANO RONALDO NI "UNTOUCHABLE"

Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane amekiri kuwa supastaa wa klabu hiyo Cristiano Ronaldo ana kila aina ya ubora na uwajibikaji unaomfanya asigusike wala kubughudhiwa (untouchable).

Zidane alisema katika mkutano wa waandishi wa habari Ijumaa kuwa Ronaldo ni "untouchable" kwa vile mafanikio aliyoyaletea na anayoendelea kuiletea klabu hiyo yanajieleza yenyewe.

Kocha huyo aliyasema hayo wakati akitangaza kuwa nyota huyo atapumzika kwenye mchezo wa La Liga dhidi ya Rayo Vallecano Jumamosi hii ili kumweka fiti kwa mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Manchester City Jumanne usiku.

"Ronaldo anataka kucheza kila mchezo. Hapendi kumpumzika na hilo ni jambo ninalolipa thamani kubwa na kuliheshimu licha ya ukweli kuwa mchezaji anapocheza mechi nyingi mfululizo mwili unachoka," alisema Zidane.

"Angependa kucheza Jumamosi, lakini hataweza kwa kuwa alipata maumivu katika mchezo wa mwisho Jumane usiku," aliongeza Zidane na kufafanua kuwa Ronaldo ni aina ya mchezaji ambaye huwezi kuthubutu kumpiga benchi pale anapokuwa fiti.

Zidane sio kocha wa kwanza kutaja wachezaji 'wasiogusika'. Mwaka 2004 wakati Jose Mourinho alipoanza kuikochi Chelsea, aliweka wazi wachezaji wake "untouchable" ambao walikuwa ni John Terry, Didier Drogba, Frank Lampard na Petr Cech.



Comments